BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma wameeleza masikitiko yao juu ya matusi na kashifa zinazotolewa na viongozi wa CCM dhidi ya wahasimu wao Chadema.
Hali hiyo ilijitokeza jana ambapo Makongoro Nyerere kuweka sera za CCM pembeni na kuanza kutoa kashfa kwa wagombea wa vyama vya siasa hususani Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa na mgombea Ubunge Benson Kigaila.
Akihutubia katika mkutano wa Kampeni wa mgombea ubunge CCM katika viwanja vya Kikuyu Kusini, Makongoro badala ya kutangaza sera za chama chake alianza kwa kashfa na kudai Ikulu hakuna makabuli hivyo Lowassa anaumwa na kuna uwezekano akafia Ikulu.
Makongoro akimnadi Anthon Mavunde, alitumia muda mwingi kutoa kashfa kwa wagombea wa UKAWA huku akidai Lowassa asichaguliwe kuwa rais kwani afya yake mbaya hivyo anaweza kutofanya majukumu yake.
Mbali na hilo amesema Ikulu siyo wodi ya wagonjwa na sehemu ya makaburi hivyo ni vyema mtu anayetakiwa kwenda Ikulu ni mtu mwenye nguvu.
“Mimi sasa sitaki kuendelea kumsema Lowassa maana akifa watasema mimi ndiye niliyemuua hata hivyo nawashangaa watu wa UKAWA wana roho ngumu sana kutembea na mtu ambaye amechoka vile.
“Chadema wanatakiwa kushitakiwa ni maajabu sana kuona na watu wasivyo na huruma wanamtesa sana baba wa watu hata hawezi kuzungumza majukwaani na sera anamwachia Lissu (Tundu),” amesema Makongoro.
Mbali na hilo Makongoro alionesha kituko alipowaambia wana Dodoma kuwa yeye (Makongoro) ni mdogo hivyo anaogopa kulala peke yake hivyo anatafuta mtu wa kulala naye.
Kutokana na hali hiyo wakazi wa Dodoma wamesema watanzania wanataka kusikiliza sera na siyo vinginevyo.