MGOMBEA Ubunge jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimebaki kinatapatapa kama mgonjwa anayetaka kukata roho, baada ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
CCM ambayo hivi sasa inakabiliwa na upinzani mkali kutoka UKAWA, inaonekana kuyumba baada ya mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa anayegombea Urais kupitia Chadema na Frederick Sumaye aliyekihama chama hicho mwezi mmoja uliopita.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni mjini hapa jana, Wenje amesema CCM ni chama kinachotarajiwa kuzikwa Oktoba 25 mwaka huu, kwani shimo lake limekwisha chimbwa na UKAWA, wanachofanya sasa ni kuhangaika namna gani kinaweza kujinasua.
Amesema CCM walililea tatizo na kuliacha likue kwa kushindwa kuwatatulia wananchi wake kero zinazowakabili, sasa wanahangaika baada mambo kuwa magumu upande wao.
Wenje amesema baada ya kuona CCM imeshindwa kuwatatulia wananchi kero zao katika jimbo la Nyamagana, alihakikisha anasimama kidete kutatua kero `sugu` za madawati ambako kwenye uongozi wake amenunua dawati 1500, ujenzi wa maabara, kununua maabara inayohama na kuondoa michango shuleni.
“Mfuko wa jimbo kwenye uongozi wangu nimepokea kiasi cha Sh. 168 milioni, fedha hizo ndizo nilinunua mifuko ya saruji kwa ajili ya maabara, kukarabati madarasa shule za msingi na kujenga vituo vya afya Isabanda, Isamilo, mahina ambavyo vinahitaji Sh. 95 milioni, kukamilika,” amesema Wenje.
Amesema awali CCM ilikuwa ikiwadanganya wananchi kuwatatulia changamato ikiwemo suala la afya, elimu na sekta ya miundombinu ya barabara kitendo ambacho wananchi wamechoka hivi sasa na wanahitaji mabadiliko.
Wenje ambaye alikuwa ni Waziri kivuli wa mambo ya ndani, amesema katika uchaguzi mkuu wa 2010 wabunge wa upinzani walikuwa bungeni waliisimamia serikali ipasavyo ikiwemo kashfa ya uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Wenje amesema Wananchi wanapaswa kuupuza maneno ya wafa maji CCM kwani lengo lao ni kutaka kuendelea kuwatawala na kuzidi kuwanyonya hivyo Oktoba 25 mwaka huu, wanapaswa kuchagua mabadiliko kuanzia madiwani, wabunge na rais.