MUIGIZAJI maarufu katika tasnia ya Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu, amewataka Watanzania wote kumchagua, Dk John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu
Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi anawania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo mpinzani wake mkubwa katika vita hiyo ni Edward Lowassa, anayegombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza katika mkutano wa kampeni wa CCM wa kumnadi mgombea huyo uliofanyika jana Jumapili kwenye Uwanja wa Jamuhuri, Morogoro na kujaza maelfu ya wananchi, mrembo huyo wa mwaka 2006 alisema utendaji kazi wa Magufuli umetukuka na hana kashfa yoyote, hivyo ndiye anayefaa kuwa Rais wa Tanzania.
“Kila Mtanzania anaujua utendaji wa Magufuli, ni mtu asiyependa mchezo kazini, hivyo huyu ndiye anayestahili kuwa kiongozi wetu na siyo mtu mwingine.
“Mimi nilishindwa katika kura za maoni, lakini nilikubali matokeo, hao wengine mliowaona wanakimbilia sehemu nyingine hawafai kuwa viongozi wetu. Ni wachafu wenye skendo za ufisadi, nawaomba Watanzania tuwe macho na watu hao na itakapofika Oktoba 25 kwa pamoja tumchague Magufuli,” alisema Wema.
