Wanafunzi wa shule ya msingi Ibugule Kata ya Khome wilayani Bahi, wametaka mbunge atakayechaguliwa kuwakilisha jimbo la Bahi, aje na mkakati utakaowaondolea adha ya kwenda shuleni, wakiwa na mifuko aina ya salfeti ambayo hutandika chini na kuikalia kufuatia ukosefu wa madawati.
Lucas Samweli (17), anayesoma darasa la sita, Shule ya Msingi Ibungule, alisema awamu hii ya uchaguzi wanatamani wazazi wao wawachagulie mbunge, atakayekuwa na ubunifu wa mipango itakayowaondolea kero, zikiwamo zinazotokana na shule nyingi jimboni humo kukosa madawati.
Tunawaomba wazazi wetu wasifanye makosa katika kupiga kura, tunataka watuchagulie viongozi watakaotuondolea kero hii, ambayo mbali na kusababisha tuchafuke, viungo vya miili yetu vinauma kwa kuandika tukiwa tumeinamisha migongo ardhini, alisema mwanafunzi huyo.
Wanafunzi wapatao watano, walipewa nafasi ya kueleza waliyonayo mioyoni, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwenye mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha ACT Wazalendo, Eva Kaka.
Kaka kwa nyakati tofauti alifanya mikutano ya kampeni katika vijiji vya Ibugule na Khome, katika Jimbo la Bahi, mkoani Dodoma.
Alisema matokeo mabaya yanayoonekana katika matokeo ya mitihani mbalimbali wanayofaya, ikiwamo ile ya kumaliza elimu ya msingi ambayo ni mitihani ya kitaifa, kiini ni mazingira mabaya ya kusomea.
Alisema ingekuwa amefikia umri wa kupiga kura, angechunguza ahadi zinazotolewa na kila mgombea udiwani na kuzilinganisha na maelezo yaliyoandikwa kwenye ilani ya chama chake, ili kujiridhisha kuwa mtazamo na msimamo wa chama cha mgombea husika, anayo dhamira ya kweli katika kutekeleza majukumu hayo.
Chanzo:Nipashe