Serikali Mkoani Njombe Imetoa Tahadhari Kubwa Kwa Walimu na Wasimamizi wa Mitihani ya Kuhitimu Darasa La Saba Iliyoanza leo Nchini Kote Juu ya Kujihusisha na Udanganyifu wa Aina Yoyote Ile.
Tahadhari Hiyo Imetolewa na Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Njombe Bwana Hans Mgaya Wakati Akizungumza na mwandishi Juu ya Maandalizi ya Mitihani Hiyo Itakayofanyika Kwa Muda wa Siku Mbili Septemba 9 na 10 Mwaka Huu.
Mgaya Amesema Kwa Mujibu wa Sheria Mwalimu Yeyote Atakayebainika Kujihusisha na Udanganyifu wa Kuiba Mitihani Pamoja na Vitendo Vingine Atakwenda Jela Kwa Miaka Takribani 20 na Kulipa Faini ya Shilingi Milioni 20.
Amesema Ili Kuepusha Usumbufu Usiowalazima Kwa Familia na Taifa Kwa Ujumla ni Vyema Walimu Hao Wakafanyakazi Yao Kwa Uadilifu Mkubwa Pasipo Kukiuka Kanuni Zilizopo.
Akizungumzia Maandalizi ya Kuelekea Zoezi la Ufanyaji Mitihani Hiyo Kaimu Afisa Elimu Huyo Amesema Maandalizi Yote Yamekwisha Kamilika na Kwamba Jumla ya Wanafunzi 15449 Katika Halmashauri 6 za Mkoa wa Njombe Ndio Wanaotarajiwa Kuanza Mitihani Hiyo leo
Pamoja na Mambo Mengine Lakini Pia Ametoa Wito Kwa Walimu Wanaolalamikia Kuidai Serikali Madai Mbalimbali na Kwamba Suala Hilo Lisiathiri Zoezi la Mitihani Hiyo Kwani Serikali Bado Inashughulikia Madai Yao.
Septemba 7 Mwaka Huu Chama Cha Walimu CWT Mkoa wa Njombe Kupitia Katibu Wake Mwalimu Romana Nyoni Kimeunga Mkono Tamko la CWT Taifa la Kuitaka Serikali Kulipa Madeni ya Walimu Hadi Ifikapo Septemba 30 Mwaka Huu Kabla Hakijachukua Hatua Zaidi.
Na Gabriel Kilamlya, NJOMBE