Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema asilimia 60 ya uvunjifu wa haki za binadamu nchini unafanywa na vyombo vya dola huku asilimia 40 ukifanywa na wananchi wa kawaida.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba amesema kumekuwa na matukio ya wananchi kuuawa wakiwa mikononi mwa askari polisi ambao kwa mujibu wa sheria za kuundwa kwake ni walinzi wa raia na mali zao.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 20 ya kituo hicho, Bisimba amesema wananchi wamepoteza uwoga kwa vyombo vya dola jambo linalopelekea kuvamia vituo vya polisi mara kwa mara, kuwatoa mahabusu, kuua polisi na kupora silaha.
Alitolea mfano mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro yaliyotokea Januari 14, 2006 katika msitu wa Pande pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam ambapo Sabinus Chigumbi (Jongo), Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva wa teksi Juma Ndugu waliuawa.
“Pia kumekuwa na vitisho na kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari vinavyoandika habari za kuikosoa serikali kama ambavyo magazeti ya Mwanahalisi, Mwananchi na The East African yalivyokumbwa na rungu la serikali” alisema.
Jaji Rufaa Mstaafu, Eusebia Munuo aliyekuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alisema sherehe hizo zimekuja sambamba na uchaguzi mkuu wa Tanzania na kukitaka kituo hicho kuhamasisha makundi yote kupiga kura.
“Kama mlivyohamasisha wakati wa zoezi la kujiandikisha, naomba muwahamasishe wananchi kutumia haki yao ya kupigakura na kuchagua kiongozi wanayemtaka na kujiepusha na vitendo vyovyote vya vurugu” alisema na kuongeza.
“Najua kituo hiki kinaheshimika na kwamba kina nguvu kubwa. Nina hakika wananchi watawasikiliza.”alisema Mmari
Mwenyekiti wa bodi ya LHRC, Geoffrey Mmari alizindua kitabu kinachoelezea changamoto za kituo tangu kilipoanzishwa hadi sasa, mafanikio yaliyopatikana na uhusiano wake na vituo vingine.
Mmari alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni Usalama wa wafanyakazi wa kituo hicho, Vitisho, kigeugeu cha wateja na kituo kutegemea wafadhili.