Mgombea urais wa vyama vinavyounda UKAWA Mh.Edward Lowassa amesema akichaguliwa kuwa rais hatakuwa na sababu ya kutegemea misaada kutoka nje kutekeleza ahadi anazotoa na sera zilizoko kwenye ilani ya UKAWa badala yake atasimamia vizuri rasilimali zilizopo kwani zinatosha kutatua matatizo ya watanzania.
Baada ya kumaliza kazi ya kufikisha ujumbe wa mabadiliko kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma ambao ni ngome na pia makao makuu ya CCM kwa mafanikio makubwa Mh.Lowasa anaingia kwa kishindo katika mkoa wa Singida na kupokelewa na umati wa wananchi wakiwa na matumaini makubwa ya kupata mabadiliko ya maisha yao kupitia ukawa chini ya Mh.Lowasa,ambaye amewaomba kumpa nafasi ya kushughulikia kero zao kwani anazijua na asilimia kubwa ufumbuzi wake uko ndani ya uwezo wake.
Mh.Lowasa ambaye awali amefanya mikutano katika wilaya ya Manyoni,Ikungi na Singida mjini anasema kupitia sera zilizoko kwenye ilani ya UKAWA na uwezo mkubwa wa viongozi na watendaji wana kila sababu ya kubadilisha maisha ya watanzania kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.
Baadhi ya wananchi na viongozi wanaounga mkono mabadiliko wamesema ubora wa sera zilizoko kwenye ilani ya UKAWA kugusa matatizo ya watanzania,UKAWA inaendelea kuwa kimbilio la,wananchi na viongozi wakiwemo wanaotoka CCM huku wakiendelea kuwaeleza wananchi faida za kubadilika na athari za kuendelea kuvumilia mateso ya CCM na ahadi zinazoonekana wazi kuwa hazitekelezeki.