Wananchi wameeleza kuchoshwa na rushwa ambayo wameitaja kama saratani inayodumaza maendeleo ya nchi na kutaka rais ajaye apambana na tatizo hilo kwa dhati bila woga .
Wakizungumza katika mwendelezo wa kampeni za kumnadi mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM Dr.John Pombe Magufuli wananchi hao wa mji wa Meatu wamesema kukosekana kwa huduma nyingi za kijamii ili kumrahisishia maisha mtanzania wa kawaida kunasababishwa na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na watendaji wa serikali jambo linaloonekana kama utaratibu wa kawaida hivyo kumtaka rais ajaye kukomesha vitendo vya rushwa kwa vitendo katika sekta zote za utoaji wa huduma.
Mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM Dr.John Pombe Magufuli kwa upande wake ameeleza kuchukizwa na vitendo vya rushwa na ufisadi kunakosababisha huduma kutomfikia mwananchi wa kawaida na kwamba litakuwa suala la kipaumbele kupambana nalo na kuwataka watendaji wajipange kutoa huduma bora na kutatua kero za wananchi.
Aidha Dr.Magufuli ameongeza kuwa serikali ya awamu ijayo endapo atapata ridhaa mbali na kutaka uchumi wa nchi uendeshwe kwa kutegemea viwanda pia atatilia mkazo katika sekta ya uvuvi na kilimo hususani cha mazao yanayowaingizia kipato kikubwa wananchi ili kukuza kipato cha kaya na taifa lakini pia kupunguza kiwango cha umasikini nchini.
Mh.Luaga Mpina akiwawakilisha wananchi wake amemuoba Dr. Magufuli atakapoingia ikulu kusaidia kutatua kero kubwa inayowakumba wananchi wa meatu ambao kwa kiasi kikubwa ni wafugaji na wakulima kuwatengea maeneo ya kilimo na ufugaji ili kupunguza migogoro iliyopo.
Dkt.Magufuli atahitimisha ziara ya kunadi ilani ya ccm katika wilaya za mkaoa wa simiyu na kuingia mkoani tabora kuhutubia mkutano wa hadhara wa kuomba ridhaa kwa watanzania waishio mkoani Tabora.