Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa mara nyingine imemtia mbaroni na kumfikisha mahakamani aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Urambo, Oscar Bulugu, kujibu mashtaka ya kuficha nyaraka za serikali na wizi wa majalada 31 ya kesi.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tabora mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Emmanuel Ngigwana.
Mawakili Simon Mashingia na Edson Mapalala, walidai kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Aprili 15 na Novemba 11, mwaka 2013, mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo.
Ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa huyo akiwa mtumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania idara ya mahakama, aliiba majalada hayo ya kesi zilizokuwa zikiendelea kusikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Urambo na kuyaficha nyumbani kwake.
Iliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo wakati akiwa amesimamishwa kazi na mwajiri wake kutokana na kukabiliwa na kesi tatu za kuomba na kupokea rushwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora.
Awali Bulugu alifikishwa mahakamani hapo mwaka 2013 na Takukuru akikabiliwa na mashtaka ya kuomba rushwa na kupokea rushwa kati ya Machi 15 hadi 22, mwaka jana, akiwa hakimu mkazi wa wilaya ya Urambo.
Ilidaiwa Machi 15 mwaka juzi, akiwa hakimu wa mahakama hiyo, alimshawishi Lucas Changala ampatie rushwa ya Sh. milioni 5 ili atoe dhamana kwa ndugu yake aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi wa fedha za Benki ya NMB.