Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema asilimia kubwa ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu yamekamilika, huku karatasi za kupigia kura zikitokea Afrika Kusini.
Aidha, tume hiyo imesema gharama za awali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kama vile wino, fulana, kofia, karatasi za kura, vibanda vya kupigia kura na vifaa vya kufungashia katika uchaguzi huo hadi sasa zimefikia Sh. bilioni 31.25.
Imesema dola za Marekani 6, 145, 882.92 sawa na Sh. bilioni 13.1 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ununuzi karatasi hizo za kura. Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Manunuzi na Menejimenti ya Lojistiki wa Nec, Eliud Njaila, wakati akizungumza, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema karatasi hizo zinatarajia kuanza kuwasili nchini Septemba 29 hadi Oktoba 15, mwaka huu.
Alisema gharama za vifaa hivyo ni tofauti na zile zilizotumiwa na tume hiyo kwa ajili ya kununulia mashine 8,000 za Biometric Voters Registration (BVR) na shughuli nzima ya uandikishaji kwenye Daftari la Wapigakura nchi nzima, ambazo kwa mujibu wa Nec ni Sh. bilioni 133.
Tume hiyo pia ilisema Sh. bilioni 85 zilitumika kulipa posho waandikishaji, wataalamu wa mashine hizo, kutengeneza kadi, karatasi, wino na vifaa muhimu wakati wa uandikishji kwenye daftari hilo nchini kote. Alitaja kampuni iliyoshinda zabuni ya wazi ya kutengeneza karatasi hizo kuwa ni Uniprint ya nchini Afrika Kusini ambayo alisema ina uzoefu mkubwa katika kazi hiyo kwani ndiyo iliyoshinda zabuni ya kutengeneza vifaa hivyo katika uchaguzi mkuu nchini humo wa Tanzania wa mwaka 2005.