Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limemshikilia na kumhoji kwa zaidi ya saa tano mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama hicho, Anthony Komu (pichani), kwa madai ya kumtisha kwa bastola Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Basil Lema.
Hata hivyo, baada ya kuhojiwa jeshi hilo lilimwachia huru Komu na kisha kulifuta jalada la uchunguzi lililofunguliwa dhidi yake baada ya mlalamikaji (Lema) kuomba shauri hilo limalizwe katika meza ya usuluhishi ndani ya Chadema.
Akizungumza nje ya Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, Komu alisema alishikiliwa na kuhojiwa kuanzia saa 5:00 asubuhi na kuachiwa saa 10:00 jioni.
“Niliwaeleza kwamba sijawahi kumiliki silaha na sina mpango wa kuimiliki wakaridhika na maelezo yangu na wakakubali mzozo uliotufikisha hapo tukaumalize nje ya vyombo vya sheria,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kwamba mgombea huyo wa ubunge Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chadema alikuwa alitumiwa ujumbe wa kuitwa polisi kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hiyo.
Agosti 18, mwaka huu wakati wa marudio ya uchaguzi wa kura ya maoni za Chadema katika jimbo hilo, Komu akiwa katika eneo la Kibosho, Moshi Vijijini alidaiwa kumtisha kwa bastola katibu huyo wa mkoa alipomfuata akitaka kujua taratibu zilizotumika kuhamisha mkutano wa uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika katika eneo la Garden, kata ya Kiboroloni, Manispaa ya Moshi.
Naye Lema akizungumzia suala hilo alisema: “Ni kweli tumemalizana na bosi wangu (Komu) baada ya kuafikiana wenyewe na kuomba polisi ikubali mambo haya yamalizwe nje ya vyombo vya kisheria kutokana na maslahi mapana ya Chadema.”
Lema alitoa taarifa polisi kuhusu Komu wiki tatu zilizopita na kupewa hati yenye namba MOS/RB/829/2015 akilalamikia kupigwa na kutishwa kwa silaha baada ya kupewa maelekezo na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema (Salum Mwalimu) kufuatilia mgogoro uliotokana na mkutano mkuu maalum wa marudio ya uchaguzi wa kura ya maoni ambao awali ulikuwa umempa ushindi Lucy Owenya.