Rais Jakaya Kikwete amesema amefanikiwa kuweka mazingira bora ya ufanyaji wa biashara hapa nchini hatua ambayo imefanya uchumi wa Tanzania kukua katika kasi inayotakiwa na hivyo kusaidia uboreshaji wa maisha ya watanzania.
Rais Kikwete amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la taifa la biashara na kusema kuwa uboreshaji huo umefanyika katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu na uwekaji wa mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara.
Naye katibu mkuu kiongozi balozi Ombeni Sefue amesema katika mkutano huo wanatumai watajadili kwa kina kuhusiana na hali ya ufanyaji wa biashara nchini ilivyo sambamba na kubuni mikakati mingine ya kuiboresha kama unavyofanya sasa mpango wa matokeo makubwa sasa-BRN.
Mbali ya kujadili mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini pia wajumbe wa baraza hilo la taifa la biashara wanatarajiwa kutumia mkutano huo kumuaga rais jakaya kikwete ambaye anamaliza muda wake wa kuliongoza baraza hilo.