Chama cha Mapinduzi Jimbo la Mbeya Mjini kimepata
pigo baada ya mgombea wake wa Kata ya Uyole, Kambi Njela , pichani juu) kufariki dunia ghafla.
Njela ambaye alianza kampeni mwezi uliopita aliugua ghafla
akiwa anaendelea na kampeni zake na kwamba dalili za ugonjwa
zilianza kwenye miguu ambayo ilionekana kupata ubaridi na
hatimaye homa kali.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya, Ephrahimu Mwaitenda
amesema kifo hicho ni pigo kubwa kwa chama hicho kwani marehemu alipita bila kupingwa
kwenye kura za maoni, hivyo tayari walikuwa na ushindi mkononi
Naye meneja wa Kampeni za CCM Wilaya ya Mbeya mjini,Charles Mwakipesile amesema kuwa marehemu alikuwa mchapa kazi na aliweza kuisimamia vizuri Ilani ya chama chake katika kata
yake na ndiyo ilikuwa inaongoza kwa maendeleo.
“Alifanya vizuri kwenye kata yake na ndiyo maana hakuweza kupata upinzani na hatimaye kupita
bila kupingwa hivyo tumempoteza mtu muhimu sana ndani ya chama na tumeipoteza kata hiyo
ambayo tayari ilikuwa mikononi mwetu”amesema Mwakipesile
Kwa upande wake Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Mbeya, Musa Zunguza amesema kutokana
na kifo hicho taratibu zinafanyika kusimamisha kampeni za udiwani kwenye kata hiyo.