Wakati mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli
wa Ukawa, Edward Lowassa akiiteka Wilaya ya Chato ambako
ni nyumbani kwa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
kwa kufanya mkutano mkubwa wa kampeni, Mwenyekiti wa
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani humo, Lucas Michael alitumia nafasi hiyo kueleza kilio cha walimu nchini na
kumponda Dk Magufuli kwa kushindwa kutetea maslahi yao.
Lucas ambaye baadaye alilieleza Mwananchi kuwa hawezi
kujuta kwa kutoa kauli hiyo hadharani akieleza “sijafanya kosa
nimesema ukweli”, akiwa jukwaani alisema Dk Magufuli
ambaye alikuwa mbunge wa Chato amewatupa walimu wa
wilaya hiyo kwa madai kuwa wananunua wenyewe chaki,
hawalipwi fedha za safari baada ya kustaafu na Halmashauri ya
wilaya hiyo inagoma kuwasomesha.
Wakati mwalimu Michael akieleza hayo, Lowassa akizungumza
katika mkutano huo uliofanyika katika stendi ya mabasi ya
zamani mjini Chato na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi
waliomsubiri kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni, aliahidi kufufua viwanda vilivyopo
mkoani humo na kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria baada ya kuelezwa kero za wananchi wa wilaya
hiyo na mgombea ubunge, Benedicto Lukanima (Chadema).
Michael aliyekuwa ameshika kipeperushi chenye picha ya Lowassa alimuomba kada mpya wa
Chadema, Tambwe Hiza aliyekuwa akizungumza jukwaani kabla ya Lowassa kufika eneo hilo,
kuwa ana ujumbe mzito kwa walimu wa Chato.
“Nimelazimika kuja hapa kuyasema yafuatayo.
Tanu ilipata nguvu baada ya Mwalimu Julius
Nyerere, Oscar Kambona na wafanyakazi wengine kuungana na Rashid Kawawa kudai uhuru wa
Tanganyika.
Bila wafanyakazi kujitetea na kudai haki yao hakuna maisha ya kweli na ya uhakika.
“Namuuliza Dk Magufuli mbona katika halmashauri yake haisomeshi wafanyakazi, mbona
wakistaafu hawapewi fedha za safari kulejea makwao, mbona walimu tunachanga fedha kununua
chaki,” alisema na kushangiliwa na wananchi.
Huku akirejea kauli ya Dk Magufuli aliyotoa hivi karibuni kwamba wananchi wamchague kwa
kuiga mfano wa alichokifanya Chato Michael alisema, “Wanasema tuchague CCM kwa kuiga Chato
sasa tunachagua nini kwa haya yanayotokea Chato.”
“Kazi ya mwalimu ni kufundisha elimu ya darasani na ya watu wazima.
Walimu wasiwe waoga
wawafundishe ukweli watu wao. Bendera ya taifa ina rangi ya njano, kijani, nyeusi na bluu huku
nyeupe ikiwa imeizunguka bendera hiyo hivyo walimu wafanye uamuzi sahihi wakati sahihi na
wakati ndiyo huu,” alisema Michael na kuibua shangwe katika mkutano huo.
Michael alilieleza Mwananchi kuwa ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Chato tangu mwaka 2007
na kwamba alianza kazi ya ualimu mwaka 1987.
“Nimekuwa mwenyekiti wa CWT hapa Chato tangu Machi mwaka huu. Sihofii kufukuzwa kazi kwa
sababu sijavunja sheria.
Jambo linaloniuma zaidi ni kitendo cha walimu wanaoonekana kuunga
mkono vyama vya upinzani kuadhibiwa na wale wanaounga mkono CCM kuachwa. Jambo hili si
sahihi kabisa,” alisema.