Mgombea urais kupitia chama cha ACT Wazalendo Anna Mgwira amesema serikali yake itashughulikia suala la uraia kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa madai ya kuwa ni raia wa nchi jirani.
Mama Mgwira ambaye alizuiliwa mara kadhaa barabarani na wananchi wakitaka awasalimie, ameyasema hayo katika kijiji cha Mnanila wilayani Buhigwe, kijiji ambacho kipo katika mpaka wa Tanzania na Burundi ambapo amewaomba wananchi kumpigia kura ili aweze kumaliza tatizo la uraia kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma huku mgombea mwenza wa urais Hamad Mussa Yusuf akieleza kuwa ACT Wazalendo inayatambua vizuri matatizo ya wananchi na imejiandaa kuyatatua ikipewa ridhaa.
Kwa upande wao wagombea ubunge katika majimbo mbalimbali ya mkoa wa Kigoma wamesema mkoa wa Kigoma unakabiliwa na changamoto mbalimbali kama maji, elimu, afya na miundombinu.
