MFALME Mswati wa Swaziland Jumatatu hii alijichagulia msichana atakayekuwa mke wake mpya, licha ya wasichana kadhaa kufariki katika ajali mbaya ya barabara wakielekea katika sherehe hiyo.
Wasichana hao, wanaokisiwa kuwa 40 walifariki baada ya lori lililokuwa limewabeba kubingiria mara kadhaa.
Kutokana na ajali hiyo, makundi ya utetezi wa haki za kibinadamu yalikuwa yameomba hafla hiyo kubatilishwa kuwa ya kuwakumbuka wasichana hao. Hata hivyo, maafisa wa kitamaduni waliokuwa wakiisimamia hafla hiyo walikataa.
Kiongozi huyo huwa anamchagua msichana mmoja kama mkewe kila mwaka katika hafla hiyo iitwayo 'Reed Dance’ ambayo huandaliwa katika kasri la kifalme, jijini Mbabane.
Maelfu ya wasichana huwa wanacheza densi mbele yake wakiwa uchi, lengo kuu likiwa ni kumfurahisha ili wachaguliwe kama mkewe.
Kulingana na takwimu wasichana 40,000 hadi 90,000 wanakadiriwa kushiriki katika sherehe ya mwaka huu.
Akiwa amevalia vazi maalum lililotengenezwa kwa ngozi ya chui, aliwasalimia wasichana hao huku wakiendelea kucheza densi kwa madaha mbele yake.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa jumba la kifalme ilisema kuwa mipango ya harusi ingali kutangazwa. Kulingana na tamaduni ya taifa hilo, msichana aliyechaguliwa hufahamika baada ya wiki chache. Familia ya msichana husika lazima ifahamishwe kuwa wawakilishi wa kifalme washamaliza matayarisho yote ya kitamaduni kwa harusi hiyo kuandaliwa.
Kutokana na ajali hiyo, Mfalme Mswati alisema kuwa serikali yake ingeziswaidia familia zilizoathiriwa.
“Tutatoa usaidizi kwa wazazi ambao waliwapoteza watoto wao katika ajali hiyo,” akasema kiongozi huyo.
Tamaduni hiyo huwa ni ya kawaida katika taifa hilo ndogo, ambayo humruhusu mfalme kumchagua mke mpya kila mwaka.
Kulingana na ripoti za tovuti ya jarida la Talk Africa, mtindo huo umekuwepo kwa muda mrefu, na unakubalika.
Wanawali wakiwa uchi
Mnamo 2012, wanawali wadogo wakiwa uchi walipitishwa mbele ya mfalme huyo kama njia ya “kusherehekea maadili na umoja”.
Densi hiyo, ambayo huitwa 'Umhlanga’ kwa lugha ya Kiswazi huvutia maelfu ya wanawake ambao hawajaolewa na wale ambao bado hawajapata watoto.
Hafla hiyo huandaliwa katika kijiji maalum cha kifalme, ambacho huitwa Lidzidzini. Kikawaida, sherehe hizo huwa zinachukua siku nane.
Wasichana ambao wanapatikana kuwa na watoto kabla hawajaolewa huwa wanapigwa faini ya ng’ombe.
Densi hiyo ilibuniwa katika miaka ya ’40 wakati taifa hilo lilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Sobhuza II. Aidha, huwa inalingana na nyingine ya awali, inayoitwa 'Umcwasho’ iliyoendeshwa na wafalme waliomtanguliwa Sobhuza.
Hafla kama hiyo, ambayo pia hufanywa nchini Afrika Kusini ilianzishwa nmamo 1991 na Goodwill Zwelithini, ambaye ni mfalme wa sasa wa jamii ya Wazulu. Densi hiyo huwa inafanyika katika makao ya kifalme ya jamii ya Zulu, yaitwao Nongoma.
Wasichana wanapofika katika makao ya kifalme, huwa wanatawanyika katika usiku unaofuata kutafuta mianzi katika sehemu zilizo karibu. Baadaye huwa wanaitumia kujifunga nayo kama matayarisho ya kucheza densi mbele ya mfalme.
Lakini kabla ya siku ya densi yenyewe, wasichana hao huwa wanapumzika kwa ili kutengeneza mavazi yao ya kitamaduni. Baadhi ya mavazi hayo ni pamoja na mikufu, njuga kati ya zingine. Wengi wao huwa wanabeba visu maalum vya kimataduni ambavyo huwa wanatumia kukatia mianzi, kama ishara ya uanawali wao.
Japo sherehe hiyo imekuwa ikikosolewa na watetezi wengi wa haki za kibinadamu, taifa hilo limeendelea kuiunga mkono huku ikionekana kama mhimili mkuu wa utamaduni wake.