Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wa kufanya kazi zao hususan katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea Uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu.
Akizungumza katika kongamano la kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha channel ten Daud Mwangosi aliyefariki akiwa kazini Rais wa umoja wa vilabu vya waandishi wa habari nchini bwana Kenneth Simbaya amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu hivyo vyombo vya dola vinapaswa kujitathmini na kuhakikisha kuwa Uhuru wa kupata habari unaheshimiwa kwa mamlaka zote.
Bw. Simbaya amesema katika kukumbuka siku hiyo muhimu ya kumbukumbu ya kifo cha Daudi Mwangosi ni muhimu kujitathimini wakati huu katika kuripoti kazi za uchaguzi mkuu hasa katika kutonyesha ushabiki wowote wa vyama.
Aidha Bw,Simbaya amesema katika hali ya kusikitisha watu ambao hawakutajwa walivamia katika nyumba anayoishi mke wa marehemu mwangosi na kumuondoa katika eneo hilo.
Marehemu Daud Mwangosi alifariki septemba 2 mwaka 2012 akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikazi huko mkoani Iringa katika kijiji cha Nyololo Mufindi na kuacha mke na watoto wanne.