Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya
Mashariki ambaye pia ni mwanasheria, Mabere
Marando amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
juzi jioni akiwa hajitambui.
Marando ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, amelazwa katika Jengo la Magonjwa ya
Moyo, wodi maalumu ya FF4, chumba namba 2.
Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, John Stephen alisema jana kuwa Marando alifikishwa
hospitalini hapo juzi jioni akiwa na hali mbaya na kwamba madaktari wanaendelea
kumfanyia uchunguzi pamoja na matibabu.
Alipoulizwa kuhusu tatizo linalomsumbua, Stephen alisema familia imeomba hifadhi
kuhusu siri za mgonjwa wao.
Mwandishi wetu alimtembelea mgonjwa huyo wodini na
kushuhudia hali yake huku mama yake mzazi akiwa pembeni, ambaye hata hivyo
hakuweza kuzungumza lolote kuhusu hali ya mwanawe.
Mke wa Marando, Redempta Lyampawe alisema mumewe hasumbuliwi na tatizo la moyo,
na kwamba madaktari wameona ni vyema akapumzishwa katika wodi hiyo.
“Sisi wenyewe hatuongei naye, hawezi kuzungumza wala kufanya lolote, tunafuata ushauri
wa daktari kwamba apewe muda wa kupumzika,” alisema Redempta.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene alisema chama
chake hakina taarifa.
Chanzo: gazeti mwananchi
