Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani
kwa kushirikiana na Kampuni ya Max Malipo wamezindua kifaa
kipya cha kielektoniki cha kufanyia malipo kwa madereva wa
magari waliovunja sheria za usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed
Mpinga alisema hicho kifaa kitaanza rasmi kutumika kesho kwa
Jiji la Dar es Salaam kwa majaribio.
“Hii imetokana na malalamiko kutoka kwa wamiliki wa magari na madereva kwamba wamekuwa
wakilipishwa faini na askari wa barabarani pasipo kupewa risiti halali ya serikali.” Alisema
Kamanda Mpinga
Aliongeza kuwa kifaa hicho kitakuwa kinagundua endapo gari ni bovu, au dereva amevunja sheria
kama vile kutovaa mkanda au kwenda kwa mwendokasi, hivyo taarifa zote zitachukuliwa pamoja
na namba ya gari na kuhifadhiwa, na dereva aliyefanya kosa hawezi kukataa kwa sababu
ataonyeshwa taarifa zote zilizokusanywa.
“Ulipaji huu wa kielektroniki hauna utofauti sana na ule unaotumika kulipia bili za umeme, maji
na ada za magari kwa njia ya mtandao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema.
Alibainisha kwamba huduma hii mpya itamuwezesha mmiliki wa gari endapo amemuazimisha
mtu gari lake kugundua kama gari lake limekamatwa na kutozwa pesa.
Kamanda Mpinga alisema dereva aliyebainika na kosa anatakiwa alipe ndani ya siku saba, na zaidi
ya siku saba atatozwa asilimia 25 ya tozo la awali na baada ya siku 14 na kuendelea atatozwa ziada
ya asilimia 50 ya tozo la awali.