Baadhi ya vijana waliomaliza mafunzi ya JKT kwenye kambi ya Burombola wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, picha na editha Karlo
Na Editha Karlo,Kigoma
MKUU wa Jeshi la kujenga Taifa Meja Jenerali Raphael Muhuga alisema kuwa jeshi hilo litaendelea kuboresha changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili kuwezesha vijana wote wanaomaliza masomo ya kidato cha sita kujiunga na mafunzo hayo kwa wakati mmoja.
Muhuga alisema hayo kwenye kambi ya JKT Burombola kikosi cha 821 katika sherehe za kumaliza mafunzo kwa vijana wa mujibu wa Taifa kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita katika mafunzo yaliyojulikana kama Operesheni Kikwete.
Kanali hotuba iliyotolewa Kanali Chacha Wanyancha aliyekuwa akimwakilisha Mkuu wa JKT katika mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo baada ya kusimama kwa miaka 20 na kurudishwa tena wamegundua kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT.
Jenerali Muhuga alisema kuwa baada ya kurudishwa kwa mafunzo hayo wamekabiliana na changamoto la ongezeko la wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kutokana na ongezeko kubwa la shule za sekondari huku miundo mbinu ya makambi mbalimbali ya majeshi ikiwa haijaboreshwa kiasi cha kutosha kuchukua wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita.
Hata hivyo alisema kuwa mkakati wa jeshi hilo kwa sasa ni kuiomba serikali kuiongezea fedha ili iweze kukabiliana na changamoto hizo na kuchukua wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita kwa wakati mmoja waweze kujiunga na mafunzo hayo.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa JKT ametoa wito kwa vijana wanaomaliza mafunzo kutumia stadi wanazopewa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kujenga Taifa badala ya kurudi mtaani na kujuhusisha na ushabiki wa kisiasa na mambo ambayo hayana manufaa kwa maendeleo yao na Taifa kwa jumla.
Akifunga mafunzo hayo MKUU wa mkoa Kigoma Issa Machibya amewataka vijana waliomaliza mafunzo ya jeshi la kujenga Taifa nchini kutumia mafunzo hayo kuwafunda vijana wenzao walio mtaani kuwa na maadili mema na kujitolea katika ujenzi wa taifa badala ya kushiriki vitendo vya uvunjifu wa maadili.
Baada ya mafunzo hayo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa vijana hao watakuwa askari wa akiba na siku zijazo ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama zitachukuliwa kutoka miongoni mwa vijana hao.
“Natoa wito kwa vijana waliomaliza mafunzo kuwa chanzo cha maendeleo katika jamii kwa kuonyesha maadili mema na utendaji uliotukuka ili kuonyesha tofauti kubwa iliyopo kati yao waliopitia JKT na vijana wenzao waliomtaani ambao hawajapitia mafunzo hayo,”Alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Awali katika risala ya vijana hao iliyosomwa na Nashorwa George wameishukuru serikali kwa kurudisha mafunzo hayo ambapo hata hivyo walisema kuwa muda unaotumika kwa mafunzo hayo kwao ni mdogo ambao unawafanya kushindwa kufanya baadhi ya mafunzo.