Watu wenye ulemavu wa ngozi Albino mkoani Mara wamesema licha ya kuwa na haki ya kuhudhuria mikutano ya kampeni kusikiliza sera za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wamekuwa wakikosa fursa hiyo kutokana na kuhofia usalama wa maisha yao.
Wamesema licha ya Serikali na vyombo vingine kukemea vitendo wa kikatili wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwemo kutekwa na kuuawa kikatili na kisha kunyofolewa baadhi ya viungo lakini bado kuna baadhi ya watu wanaendeleza vitendo hivyo hali ambayo inawaogopesha kwenda kwenye mikutano ya kampeni.
Walemavu hao wameyasema hayo wakati wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama cha walemavu wa ngozi (Albino) TAS wilayani Bunda, uliofanyika katika ukumbi wa Hongera uliyoko mjini Bunda.
Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) TAS mkoani Mara, Bi. Helena Paulo, aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, pamoja na katibu wa TAS wilayani Bunda, Melisiana Levocatus, wanasema kuwa Albino wao pia wanayo haki ya kuhudhuria kwenye mikutano hiyo, ili kusikilza sera za wagombea, lakini wengi wao wamekuwa wakishindwa kuhudhuria kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Wanasema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi ya watu kuendelea kuwatishia maisha yao na kwamba ni vema sasa serikali na jamii kwa ujumla, wakazidi kuimarisha ulinzi na usalama wao, kwani wao pia ni wananchi ambao wanastahili kuhudhuria kwenye mikutano hiyo na kusikiliza sera za wagombea na ilani za vyama vyao.
Wanasema kuwa hali hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kusikiliza sera za wagombea pamoja na ilani za vyama vyao, ili wakati wa kupiga kura waweze kuchagua viongozi wanaowataka kwa usahihi kabisa.
Katika hatua nyingine wanasema kuwa wamekuwa wakinyanyapaliwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali pindi wanapokwenda katika ofisi zao kwa ajili ya kutafuta huduma mbalimbali, ikwa ni pamoja na kuyanyanyapaa majarida yenye habari zinazohusu watu hao wenye ulemavu wa ngozi (Albino)
Katika uchaguzi huo Happynes Manobi kwa jina maarufu Mayo, aliyenusurika kuuawa baada ya kutekwa na watu wasiojulikana hivi karibuni mjini Bunda, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa TAS Wilayani Bunda, katibu amechaguliwa Melesiana Levocatus na mweka azina amechaguliwa Sabato Minith.
Waliochaguliwa katika kamati ya utendaji ni pamoja na Nyamambara Busagi, Hidaya Masaba na Samwel Mohamed, mwakilishi Mkoa ni Naomi Joseph na mjumbe taaluma katika wilaya ya Bunda ni Alex Mwelangalo.