

Ni kauli ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Jakaya Mrisho Kikwete kwa wakazi wa eneo la Msanga mkuu na Mtwara mjini kudhihirisha kutimizwa kwa ahadi yake ya kuwapatia kivuko ambacho amekizindua rasmi kwa lengo la kuwasaidia katika shughuli za kijamii na maendeleo kutokana na wananchi hao kukosa usafiri wa uhakika kutoka Msanga mkuu - Mtwara mjini jambo lililowalazimu kutimia mitumbwi na baadhi yao kufariki dunia ambapo kivuko hicho kimekuwa ni zawadi tosha kwa wananchi wakati rais akiwaaga kutokana na muda wake wa kuwa madarakani kumalizika huku akiwasisitiza kukitumia kwa ajili ya maendeleo.
Waziri wa ujenzi Dr John Pombe Magufuli ambaye pia ni mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha mapinduzi aliyembatana na rais Kikwete ameelezea adha waliyokuwa wakiipata wananchi hao wa Msanga mkuu ikiwalazimu kuzunguka kwa takribani kilomita 21 katika safari ambayo ingetumia dakika 7 pekee kutokana na kutokuwepo kwa kivuko hicho.
Akielezea mradi wa kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba takribani tani hamsini kilichogharimu shilingi bilioni 3.3 fedha za ndani afisa mtendaji mkuu wa tamesa amesema kivuko hicho kimetengenezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa huku mbunge wa mtwara vijijini hawa ghasia pamoja na wananchi wakielezea namna kivuko hicho kitakavyoleta ukombozi kwa wakazi wa Msanga mkuu na Mtwara kwa ujumla.
Katika tukio jingine rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la mradi wa nyumba zinazojengwa na shirika la nyumba la taifa NHC katika eneo la shangani mkoani Mtwara ambapo mkurugenzi wa shirika hilo la nyumba Nehemia Mchechu amemuelezea pia rais juu ya mradi wa mji wa kawe unaotarajiwa kuwa wa kipeke katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki na kati.