Na Nathaniel Limu, Singida
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ikungi mkoani Singida,kimemvua uanachama na kumfukuza kwenye nafasi hiyo ya uenyekiti, Christina Samwel Hamisi, kwa tuhuma ya kukiuka sheria, kanuni na taratibu.
Hayo yamesemwa na Katibu CCM wilaya ya Ikungi mkoani Singida,Aluu Segamba,wakati akitoa uamuzi huo wa vikao vya chama tawala mbele ya waandishi wa habari mjini hapa.
Segamba alisema Christina alipobwagwa kwenye kura za maoni za ubunge viti maalum CCM, alilalamikia kitendo hicho hadi kwenye vyombo vya habari, kitendo hicho cha kubwagwa na kutishia kuhamia CHADEMA.
“Dhamira yakeya kuhamia CHADEMA aliitekeleza mapema lengo lake ikiwa ni kugombea udiwani viti maalum kupitia tiketi ya CHADEMA.Huko CHADEMA nako aliangukia pua kwa kuambulia kura sifuri(0)”alifafanua.
Akifafanua zaidi,alisema Christina amejifukuza na kujivua uanachama yeye mwenyewe kutokana na kitendo chake cha kuhama CCM na kuhamia CHADEMA.
“Kwa sasa nafasi ya mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ikungi, nafasi hiyo ipo wazi kwa sasa.Tunachofanya kwa sasa ni kufuata sheria,kanuni na taratibu za chama kuitangaza nafasi hiyo ili tuweze kuziba pengo”,alisema Segamba.
Katika hatua nyingine, Segamba alisema Elibariki Emmanuel Kingu,ameshinda nafasi ya ubunge jimbo la Singida magharibi kwa kupata kura 4,759.Kingu amewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora.
Alitaja wengine na kura zao kwenye mabano, kuwa ni Dinawi Samwel Gabriel (901), Hamisi Shaban Lissu (1,918), Willson Elisha Nkhambaku (2,836), Dk.Hamisi Hema Mahuna (1,013), Dk.Grace Khwaya Puja (762), Yona Daud Makala (252) na Hamisi Hassan Ngila (384).
Kwa upande wa jimbo la Ikungi mashariki,katibu huyo alisema Jonathan Andrew Njau ameshinda kwa kupata kura 6,312 na kufuatiwa kwa mbali na Mdimi Emmanuel Hongoa aliyepata kura 1,564.
Alitaja wengine na kura zao kwenye mabano kuwa ni Hamisi Abeil Maulid (1,409), Jacob Theophil Kituu (515), Emmanuel Japhaet Hume (454) na Martin Labia Lissu (1,291).
Katibu wa CCM wilaya ya Manyoni, Dafroza Lucas, alisema nafasi ya ubunge jimbo la Manyoni magharibi, limechukuliwa na Mwenyekiti wazazi wilaya ya Manyoni,Yahaya Omari Masare aliyepata kura 6,164 na kufuatiwa na mbunge aliyemaliza muda wake,John Paulo Lwanji,aliyepata kura 2,651.
Dafroza alitaja wagombea wengine na kura zao kwenye mabano kuwa ni Elphas Eammanuel Lwanji (1,387),Jamal Juma Kuwingwa (403), Jane Lucas Likuda (396) Mojammed Juma Makwaya (280), Yohana Stephen Msita (482),Moshi Musa Mmanywa (508), Adimini Mwakapalila (Msokwa (985),Dk.Mwanga Mkayangwa (1,745), Rashid Ramadhani Said (199) na Francis Pius Shaban (80).
Jimbo la Manyoni mashariki, alisema nafasi ya ubunge imechukuliwa na Daniel Edward Mtuka (6,792) akifuatiwa kwa karibu na Dk.Pius Stephen Chaya (6,270).
Dafroza alitaja wengine na kura zao kwenye mabano kuwa ni,Gaitani Francis Romwald (1,542),Joseph Meshack Chitinka (592), AlexNyamejo Manonga (433), Jumanne Bosco Mtemi (715) ,Eng.Horold Jackson Huzi Mtyona (1,212) na Gaitaini Francis Romwald (1,542)