Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi rais Jakaya Kikwete amefungua kikao cha kamati kuu ya chama hicho ambapo pamoja na mambo mengine kikao hicho kitajadili na kupendekeza majina ya wagombea ubunge na wawakilishi ambao watapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika October 25 mwaka huu.
Ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine amewaagiza wajumbe wa mkutano huo kufanya kazi iliyowaleta kwa kuzingatia weledi na muda kwani watanzania wanasubiri kujua ni kina nani watapeperusha bendera katika uchaguzi mkuu ujao.
Awali kabla ya kumkaribisha mwenyekiti huyo kufungua kikao cha kamati kuu katibu mkuu wa CCM Abrahman Kinana alikieleza kikao hicho kuwa wajumbe wanaopaswa kuhudhuria ni 32 lakini waliopo ni 25 hivyo akidi naruhusu kikao hicho kuendelea.
Muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho katibu wa NEC itikadi na uenezi Nape Nnauye anatoa taarifa kuwa kamati kuu imeagiza uchaguzi wa kura za maoni katika majimbo matano urudiwe kutokana na kasoro ambazo hakutaka kuziweka wazi huku akiyataja majimbo hayo kuwa ni Busega, Kilolo, Ukonga, Rufiji na Makete.
Kikao hicho kinatarajiwa kukaa kwa siku mbili na kutoa maamuzi na kisha kufuatiwa na kikao cha halmashauri kuu ya CCM NEC ambayo itakaa kujadili na kupitisha maamuzi ya vikao ambavyo vimetangulia vya chama hicho.