Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani nchini naibu kamishna Mohamed Mpinga ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha kuwa elimu ya usalama barabarani inatolewa kikamilifu kwa waendesha pikipiki almaarufu bodaboda la sivyo nguvu kazi ya taifa itatoweka kufuatia idadi ya usafiri wa pikipiki kuzidi kuongezeka siku hadi siku.
Mpinga ametoa agizo hilo wakati akizungumza na waendesha bodaboda wa jiji la Tanga wakati wa ufungaji wa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa ajili ya kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya watanzania kwa sababu ya kushindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Tanga mratibu mwandamizi wa polisi Abdi Issango amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka jana hadi sasa wameshatoa mafunzo kwa waendesha pikipiki zaidi ya 340 katika jiji la Tanga idadi ambayo ni kubwa na imesaidia kupunguza ajali za barabarani.
Kufuatia hatua hiyo afisa habari wa kampuni ya bia nchini TBL ambayo kwa kushirikiana na jeshi la polisi ndio walioratibu zoezi la elimu ya usalama barabarani kwa bodaboda Bi, Dorisi Malulu amewataka wasafirishaji wa pikipiki kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawajapata elimu hiyo ili na wao waweze kunufaika kufuatia jeshi la polisi kutoa elimu hiyo mara kwa mara ili kupunguza ajali za barabarani.