MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ametangaza kung’atuka wazifa wake, kwa kile alichoeleza, “kuwa kikwazo” katika harakati za kukindoa madarakani Chama Cha Mapinduzi.
Amesema, ndani ya CUF haaminiki tena katika mapambano ya sasa ya kutaka kukiondoa chama tawala mamlakani, hivyo “nimeamua kujiweka pembeni” ili kazi hiyo iweze kufanyika kwa ufasaha.
Amesema, “Katika hali halisi iliyopo ndani ya uongozi wa chama chetu, mimi naonekana kikwazo. Naonekana nakwamisha mapambano ya ukombozi. Kwamba siwezi kuwa na mchango wa maana kama mwenyekiti katika mapambano ya kudai haki sawa kwa wote katika kipindi hiki.”
Aidha, Prof. Lipumba amesema, ameamua kujiuzulu kwa kuwa baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamewakaribisha wanachama na viongozi wa CCM waliokuwa mstari wa mbele kupinga Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alikuwa mmoja wa wenyeviti wanne wanaounda UKAWA, waliokutana na waandishi wa habari makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam na kutangaza kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya vyama vyao.
Wenyeviti wengine walikuwa James Mbatia, NCCR- Mageuzi; Emmanuel Makaidi, National League Democrat (NLD); na Freeman Mbowe, Chadema.
Prof. Lipumba ndiye aliyetoa tamko la kumkaribisha Lowassa kujiunga na UKAWA ili kutimiza adhima yao ya kukiondoa CCM madarakani.
Tayari Lowassa amejiunga na Chadema na kutangazwa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Naye Juma Duni Haji, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CUF, ametangazwa kuwa mgombea mwenza, baada ya kutimiza takwa la kikatiba la kujiuzulu nyazifa zake na kujiunga na Chadema.
Chanzo:mwanahalisi online