Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Chiku Abwao ndiye atakayepeperusha bendera ya ACT kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa mjini katika uchaguzi mkuu ujao, huku akitamba kwamba atambwaga mbunge anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Mbali na Abwao aliyejiunga na ACT Wazalendo hivi karibuni, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema, Abuu Changawa naye ameiacha Chadema na kujiunga ACT Wazalendo, huku akitangaza kuwania udiwani katika Kata ya Mivinjeni, mjini hapa.
Abwao aliyewahi kuwa mbunge wa NCCRMageuzi, alisema; “Nimeondoka Chadema baada ya kubanwa kila kona na Mchungaji Msigwa akidhani kwamba mimi nilikuwa Chadema kwa sababu ya kutaka cheo.”
Alisema pamoja na kunusurika maisha yake wakati akipigania ushindi wa Mchungaji Msigwa 2010, mahusiano yao kisiasa yamekuwa mabaya kwa kipindi chote kwani kila alilokuwa akijaribu kulifanya kwa niaba ya chama hicho alitafsiriwa analenga kugombea ubunge jimbo la Iringa Mjini.
Alisema ili kumuonesha nguvu yake kisiasa na kwamba yeye sio mwanasiasa anayetaka tu uongozi lakini mwenye dhamira na maono ya dhati ya kusaidia kuleta mabadiliko nchini atagombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini kupitia ACT Wazalendo.