Rais Kikwete asaini miswada 10 iliyopitishwa na Bunge

Rais Jakaya Kikwete, amesaini miswada mitano ya sheria, iliyopitishwa na Bunge la 10 Julai, mwaka huu.
Imo iliyozua tafrani na kusababisha wabunge 45 wa Ukawa kutimuliwa bungeni na wengine kususia mkutano wa 20.
Katika tukio la kihistoria lililofanyika Ikulu, jana na kuhudhuriwa na mawaziri, watumishi wa wizara na wadau wa mafuta na gesi, Rais alisaini miswada hiyo baada ya mawaziri husika kuwasilisha maelezo ya miswada hiyo.
Miswada hiyo ni wa sheria ya mafuta, sheria uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, muswada wa sheria ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi pamoja na muswada wa sheria ya Tume ya walimu.
Vile vile muswada wa sheria ya usimamizi wa masoko ya bidhaa yote ya mwaka 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa Tanzania kwa miswada mitano kusainiwa katika hadhara kubwa ya watu.
Alisema miswada ya sheria ya gesi na mafuta inaweka utaratibu mzuri wa kimfumo, kisheria na udhibiti mzuri wa kusimamia uchumi wa gesi na mafuta, kujibu kilio cha Watanzania kuwa rasilimali ziwanufaishe na kizazi kijacho.
Balozi Sefue alisema pia watanzania wataunganishwa na ulimwengu wa gesi kwa biashara watakazoanzisha na kutekeleza katika uchumi huo, ikiwa ni pamoja na kuwa na uchumi nyumbulifu katika kulinda mahitaji ya vizazi vijavyo na cha sasa.“Tunafanya walichofanya wengine duniani na kuepuka yaliyoleta matatizo katika nchi nyingine,” alisema Balozi Sefue.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema muswada wa sheria ya mafuta unalenga kuleta sheria mpya ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta nchini kwenye masuala ya utafutaji; uendelezaji; uzalishaji; usafirishaji; uagizaji; uchakataji; uhifadhi na biashara ya mafuta na gesi asilia nchini.
“Malengo ya muswada wa sheria ni kuimarisha usimamizi wa sekta ili kuhakikisha maslahi ya nchi katika tasnia ya mafuta yanalindwa kikamilifu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kuweka mfumo madhubuti wa kisheria utakaoimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini kupitia sheria moja,” alisema  na kuongeza:
“Masuala muhimu ni kuweka utaratibu ambao serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitashirikiana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa vitalu vya mafuta na gesi katika yaliyo kwenye maeneo yanayugusa pande zote mbili,” alibainisha.
Simbachawene alisema sheria hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Pura) ambayo itasimamia shughuli zote za udhibiti katika masuala ya kiufundi na kibiashara katika mkondo wa juu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo