BAGAMOYO
Mkazi wa kijiji cha Magomeni Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani,
Khamisi Tanga (46), ameota matiti katika hali isiyo ya kawaida
ikidaiwa imesababishwa na kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi
ARV’S.
Akizungumza na waandishi wa habari
waliokwenda Wilayani humo kufanya utafiti kuhusu utekelezaji wa sheria
ya Ukimwi na Chama cha Waandishi wa habari za Ukimwi (AJAT),Khamisi
(Pichani) alisema alipatwa na mkasa huo miaka mitatu iliyopita.
Akisimulia namna alivyoanza kuugua alisema awali aliona
matiti yake yakiongezeka ukubwa kila kukicha lakini hakujua kama
lingeweza kuja kuwa tatizo kubwa kama lilivyo sasa.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ilimbidi kwenda
kliniki anayohudhuriaga kupata dawa na kuwaeleza manesi ambapo walimjibu
kuwa imesababishwa na dawa anazotumia na hivyo kulazimika kukatizwa
dozi hiyo na kupewa aina nyingine.
Hata hivyo Khamisi alisema kwamba pamoja na kubadilishiwa
dozi hajaona kama kuna mabadiliko yoyote aliyoyapata na kuongeza kwamba
hivi karibuni alipewa dawa nyingine ambazo kati ya hizo kuna zile ambazo
zilimsabishia matiti na tayari ameanza kupatwa na maamuvu aliyokuwa
akisikiaga awali wakati matiti yalivyokuwa yanaanza kuota.
Kwa mujibu wa Khamisi ameshahangaika kupata matibabu hadi
Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili lakini hadi leo hajapatiwa tiba stahili
ya kumaliza tatizo hilo.
“Jamani Watanzania naomba wanisaidie kwa njia yoyote ile ili
niondekane na hali hii kwani inanidhoofisha sana na kunikosesha raha
hasa mbele ya wanaume wenzangu.
Kwani hapa navyoongea na nyie waandishi nilipimwa hadi kansa na
matiti ndio kama hivyo mnavyoyaona yanaendelea kukua na huniuma sana
hasa wakati ninapolala,”alisema kaka huyo.
Pia alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Jakaya Kikwete kumsaidia
ili arudi katika hali yake ya uanaume kwa kuwa maisha kwa sasa kwake
yamezidi kuwa magumu kwa kuwa hawezi kufanya kazi yoyote kutokana na
hali hiyo.
Kwa upande wa mtaalam wa magonjwa, Dk. Dina
Komakoma,akielezea kuhusu sababu za kutokewa kwa hali hiyo kwa wagonjwa
wenye maambukizi ya VVU ni jambo la kawaida japo hutofautiana.
Dk. Komakoma alisema wengine hujikuta wakinenepa au wakikonda
sana na hili la Khamis sio mtu wa kwanza kupatwa na hali hiyo na
kuongeza kwamba inapotokea mgonjwa akapata hali tofauti kama hiyo
anapaswa kusitishiwa dawa.
SOURCE DAILY NKOROMO BLOG