KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nzega, Mkoa wa Tabora, Maselina Mihayo, amelazimika kuwalipa madiwani wa halmashauri yake deni la Sh. milioni 108 kati ya Sh. milioni 200 ambazo halmashauri yake inadaiwa baada ya madiwani wake kutishia kufunga ofisi zake.
Chanzo cha uhakika wilayani humo, kimedokeza kuwa madiwani hao, kwa muda mrefu sasa, wamekuwa wakidai fedha zao hizo zinazotokana na posho zao za kila mwezi pamoja na posho za vikao, hali ambayo iliwalazimu wiki iliyopita kutishia kufunga ofisi hizo za Kaimu Mkurugenzi wao, kama moja ya njia ya kushinikiza malipo hayo.
Akizungumza Mihayo amekiri kupata misukosuko hiyo kutoka kwa madiwani wake hao na kwamba kwa sasa ameamua kuandaa malipo hayo ya Sh milioni 108 wakati ofisi yake ikiendelea na mchakato wa kutafuta kiasi kingine cha fedha kilichobakia ili madiwani hao waweze kulipwa kabla ya kumaliza muda wao.
Kipindicha miaka mitano ya udiwani na ubunge, kinatazamiwa kumalizika wiki hii baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungao kuvunjwa Julai 9, 2015 ili kutoa nafasi kwa madiwani na wabunge hao kuanza rasmi mchakato wa kutetea nafasi zao hizo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mmoja wa madiwani hao ambaye hakupenda jina lake litajwe ndani ya Gazeti Mtandao hili, deni hilo la Sh milioni 200 ambazo madiwani hao wanaidai halmashauri zao, kwa kiasi kikubwa limetokana na malimbizo ya posho zao za kila mwezi, posho za vikao pamoja na madai mengine mbalimbali ya kiutendaji.
credits:fikrapevu
