KINGUNGE AIBUA MJADALA, ARUSHIWA KOMBORA ZITO

KAULI ya mwanasiasa wa zamani Kingunge Ngombale-Mwiru kumshambulia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye kuhusu maamuzi ya vikao ndani ya chama hicho, ameibua mjadala kutoka kwa wajumbe wa vikao hivyo, wanaohoji anachokitetea mzee huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajumbe hao wamehoji kinachomsukuma Kingunge kupigana kufa na kupona kumtetea mmoja wa makada bila kuzingatia maslahi ya chama na taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, Nape alisema Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM kuingia katika Vyombo vya Dola, toleo la Februari 2010 hazitoi nafasi kwa mgombea wa nafasi ya urais kukata rufaa.

Hata hivyo, Kingunge akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba mgombea anaweza kukata rufaa bila kutoa mifano wala nukuu ya kanuni husika.

Mmoja wa wajumbe wa NEC aliyepo Dodoma alisema mkakati wa baadhi ya wagombea ni kuvuruga vikao baada ya kuanza kukata tamaa.

“Wapo wanachama waliwahi kukata rufaa huko nyuma, akiwamo Lowassa mwenyewe 1995 kupitia makada wengine akina Galus Abeid na Yusuf Makamba, lakini Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema kwamba kazi ya vikao vya maamuzi ni kupunguza idadi ya wagombea si kuongeza majina,” alisema mjumbe huyo na kuongeza;

“Mifano mingine ni mwaka 2005 ambapo Mzee John Samwel Malecela alikata rufaa kupinga kuenguliwa katika nafasi ya kuwania urais kupitia CCM na alipoomba kujieleza ndani ya NEC alijibiwa kwa dakika tatu tu kwa Mkapa kuzungumzia mambo mawili tu ikiwamo suala la umri kuwa mkubwa na kukumbushia kukataliwa kwa Malecela na Mwalimu Nyerere.”

Alisema katika mchakato huu unaoendelea, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alipoingizwa katika kundi la wataka urais sita waliosimamishwa na CCM mwaka 2014, aliamua kukata rufaa kupinga kuhukumiwa bila kuzingatia uzito wa makosa anayotuhumiwa nayo, lakini hadi sasa hakuwahi kujibiwa wala kujadiliwa na badala yake CCM iliendelea na mchakato wake.

Mjumbe huyo mkongwe alisema katika hali ya kawaida, vikao vya maamuzi vinakuwa na ratiba ambayo wakiruhusu kukata rufaa, italazimika kusitisha shughuli zote kwa muda usiojulikana.

“Kinachofanywa na Kingunge ni kutafuta uhalali wa kukata rufaa ili kuvuruga mchakato, ili vikao vya NEC na Mkutano Mkuu usifanyike wakati kanuni ya tano imekaa kimya kuhusu rufaa katika vikao vya uchujaji na uteuzi,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mzee Kingunge akionekana kumtetea mmoja wa wagombea alitoa mfano wa Mzee Malecela bila kueleza jinsi Mkapa alivyozima hoja ya Malecela alipopewa nafasi ya kuzungumza (si kukata rufaa) ndani ya NEC.

Alisema tayari baadhi ya wafuasi wa wagombea wameanza kueneza taarifa kwamba Nape amefukuzwa uongozi na kuvuliwa uanachama kwa kumzibia nafasi mgombea wao na kwamba mapendekezo hayo yametolewa na Kingunge.

"Kingunge ambaye watu wengi wanaamini kwamba ni muumini wa Mwalimu, leo anaenda kinyume kabisa na misimamo yake wakati wa uhai wa Baba wa Taifa," alisema.

Kada huyo alienda mbali zaidi akisema kwamba hizo  hasira na visasi vya Kingunge vinatokana na migogoro katika kampuni zake za ujenzi na ukusanyaji ushuru katika kituo cha mabasi Ubungo.


Chanzo:Gazeti la majira


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo