TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema inakusudia kuwafikisha Mahakamani wananchi zaidi ya 100, wa Mkoa wa Njombe, baada ya kubainika kuwa walijiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Naibu katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Daftari na Tehama, Daktari, Sisi Kariali, amesema kwamba wananchi hao wamebainika kwa kutumia teknolojia inayotumiwa na tume hiyo na kwmaba zoezi hilo litaendelea katika maeneo yote nchini.
Aidha, amesema picha na majina ya watuhumiwa hao yamepelekwa kwenye idara zinazohusika huku akiwaonya wananchi ambao bado hawajaandikishwa kuacha kufikiria kwamba wanaweza kujiandikisha zaidi ya mara moja bila kubainika.
Amesema hadi sasa tume imekamilisha uandikishaji katika mikoa mitano (5), ambayo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa na Njombe na kwamba hadi kufikia Juni 18, 2015, itakuwa imekamilisha uandikishaji kwenye mikoa mingine 8.