Wakati wa uwekaji jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mbalatse —Lupombwe wilaya ya Makete Mkoani Njombe wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja, Serikali imesema kiasi cha shilingi Bilioni 9 zimetengwa kujenga miradi ya Maji wilayani Makete.
Akizungumzia hali ya huduma ya Maji wilayani humo, Mhandisi Sanga alisema, Wizara inahakikisha inajenga miradi mingi kadri itakavyowezekana na pia inaboresjha miradi iliyopo ili kuwasogezea wananchi huduma ya maji.
“Tunaipitia miradi ya Ludilu- Kijombo, Maranduku na Ukange ili kuiongezea ubora zaidi na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji ili tuweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na mwezi ujao tutatoa Shilingi Milioni 400 ili kuboresha miradi hii,” alisema Mhandisi Sanga.
Vilevile amebainisha kuwa kwa mwaka huu wa fedha Wizara itaendelea kutoa fedha za kujenga miradi ya Ujuni-Nkenja, Magoye, Lupalilo na Tandala, Ipelele na Ipepo, Luwumbu, Utanziwa, Kidope Madihani, Usalimwani Mfumbi na Ruaha.
“Lakini ipo miradi inayoendelea ikiwemo ya Ikete, Uganga, Idende-Unenamwa, Lupila, Utweve Mbalache-Lupombwe hii pia tutaendelea kuitaia fedha ili iweze kukamilika na itoe huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hii ya Makete,” alisema Mhandisi Sanga.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji inajenga zaidi ya miradi 1,000 katika maeneo mbalimbali kote nchini lengo likiwa ni kuwasogezea huduma ya majisafi na salama wananchi wake.
Katika Taarifa iliyosomwa na Mdiakonia Elikana Kitahenga imeeleza kuwa Mradi huo umejengwa kwa ushirikiano wa wahisani kutoka Humberg Ujerumani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Mashariki usharika wa Lupombwe, Wakala wa maji safi Vijijini (RUWASA) pamoja na Nguvu za wananchi.