Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Njombe kimejipanga kuchukua majimbo yote matano ya mkoani hapa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Emmanuel Masonga alisema kuwa katika kuhakikisha ushindi huo, chama hicho kinajipanga kwa ajili ya kuwapata wagombea wanaokubalika na watu.
“Tumejipanga vizuri kuchukua majimbo yote ya Mkoa wa Njombe, tuna watu makini na wasomi waliotangaza nia kwa ajili ya kugombea na tuna imani kuwa kupitia hapa, tutapata watu wazuri watakaopeperusha bendera ya chama hicho na tutawaunga mkono,” alisema Masonga.
Aliwataka wakazi wa majimbo yote ya Mkoa wa Njombe ambayo kwa sasa yanawakilishwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukipa kura chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ili kupata uwakilishi madhubuti na wenye tija kimaendeleo.
Alisema wakazi wa Njombe hasa wa Jimbo la Njombe Kusini linaloongozwa na Spika wa Bunge Anne Makinda, kwa muda mrefu wamekosa uwakilishi wa kweli, baada ya mwakilishi wao kushindwa kuwatembelea jimboni na kujua matatizo kutokana na shughuli nyingi zinazomkabali.
“Makinda anafika kwenye misiba na wakati wa kampeni tu hana muda wa kusikiliza matatizo ya wananchi,” alisema Masonga.
Majimbo mengine yanayowaniwa na Chadema ni Wanging’ombe linaloongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge na Jimbo la Makete la Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Binilith Mahenge, Njombe Kaskazini linaloongozwa na Deo Sanga na Jimbo la Ludewa aliko Deo Filikunjombe.
Hata hivyo, Masonga alisema ikilinganishwa na wabunge wengine, Filikunjombe kuna jambo alilofanya katika jimbo la Ludewa, lakini napo bado kuna kazi ya kufanya ndiyo maana Chadema wanajipanga kulichukua.
“CCM katika Ilani yao waliahidi kupeleka lami Ludewa na Makete, lakini wameshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo kwa sasa sisi wa Chadema tunawaomba wananchi watupe ridhaa tuwawakilishe ili tukaisimamie Serikali kwa ajili ya maendeleo baada ya wabunge wa CCM kushindwa,” alisema Masonga.
Wakati Chadema ikiweka mikakati hiyo, CCM wameendelea na kampeni zake za chini chini kuyatetea majimbo hayo.