Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Lulandala Msemwa akihutubia kwenye Mkutano huo
Na Eddy Blog, Makete
Wananchi wa kata ya Tandala wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuacha woga na kubadili fikra zao katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kuhakikisha wanakichagua chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA ili kiingie Ikulu mwaka huu
"Hakuna haja ya kuendelea kukumbatia chama cha mapinduzi (CCM), kwa sasa kimechoka na pia kama kingekuwa mtu sasa hivi kimefikia umri wa kustaafu, tukistaafishe sasa katika uchaguzi wa mwaka huu" ndivyo alivyosema mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe Lulandala Msemwa katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika jana katika kata ya Tandala
Amedai mbali na yote hayo pia jimbo la Makete ambalo linaongozwa na mbunge wa CCM, ni jimbo ambalo lipo kwenye mkakati wa Majimbo matatu ya mkoa wa Njombe ambayo lazima yatachukuliwa na CHADEMA mwaka huu
Amesema chama cha mapinduzi kwa sasa hakifuati misingi ya chama hicho iliyowekwa na waasisi wa chama hicho akiwemo mwalimu Nyerere, na badala yake kimekuwa chama cha watu binafsi wenye kujipenda wenyewe na kuwaacha wananchi wakiendelea kukikumbatia
Msemwa amesema zamani ilikuwa watoto wa vigogo wakubwa wa nchi hii hasa kwenye utawala wa mwalimu Nyerere walikuwa wakisoma shule za serikali na watoto wa walala hoi, tofauti na ilivyo sasa watoto wa viongozi wa nchi hii wanasoma kwenye shule tofauti
Katibu wa Chadema mkoa wa Njombe Bw. Nyagawa amesema kwa sasa ni muda wa mabadiliko na hivyo wanatandala waache woga na wabadili fikra zao kwa kujiunga na Chadema kama walivyofanya wananchi wa maeneo mengine akitolea mfano wilaya ya Momba ambayo inaongozwa na chadema wa zaidi ya asilimia 70
Mkutano huo umehusisha viongozi wa kata ya Tandala, wilaya na Mkoa wa Njombe ambapo akiuthibitishia mtandao huu, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Makete Bw. Ngogo amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Makete wanachama 61 wamejiunga na chama hicho huku zaidi ya vijana 20 wakujitolea wakijitokeza kwa ajili ya kupatiwa mafunzo maalum na chama hicho ya namna ya kulinda kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu