Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakieleza hofu ya Uchaguzi Mkuu kuahirishwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesitisha mchakato wa kuandikisha wapigakura mkoani Mbeya uliopangwa kufanyika kuanzia Mei 5 hadi itakapotangazwa tena.
Tayari kazi hiyo inaendelea kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa ambako kazi hiyo pia ilianza kwa kusuasua, na NEC ilitarajiwa kuongeza kasi ya uandikishaji kwa kuingia mikoa ya Dodoma, Katavi na Mbeya ambako mpango huo umesitishwa kwa muda usiojulikana.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Lazaro Samweli alisema walipewa taarifa za kusitisha uandikishaji hadi hapo watapotaarifiwa tena licha ya Tume hiyo kupeleka vifaa vya BVR.
Mwezi uliopita, Nec ilitangaza kwamba ingeanza kazi hiyo ya kuboresha Daftari la Wapigakura mkoani hapa Mei 5, jambo ambalo lilisababisha uongozi wa jiji utangaze nafasi za kazi ya kuandikisha kwa wenye ujuzi wa kompyuta.
“Kabla ya Mei 4, ofisa kutoka Tume ya Uchaguzi alikuja akatuambia tusimamishe mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia hadi hapo tutakapotaarifiwa, lakini vifaa tulishavipokea, hivyo tunawasubiri wao watakavyotuelekeza taratibu zao kwa mara nyingine tena,”Dk Samweli.
Alisema walipokea mashine 86 za BVR kutoka NEC na kwamba mashine 15 kati ya hizo ni kwa ajili ya mafunzo ya waandikishaji na 71 zinazosalia zitakuwa maalumu kwa kazi yenyewe ya kuandikishia.
Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakituhumu kuwa kusuasua huko kwa kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura ni mpango wa kutaka Serikali ya Awamu ya Nne iongezewa muda kwa kuwa haijajiandaa kukabidhi madaraka.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hakuwa na taarifa za kusitishwa kwa uandikishaji mkoani Mbeya, lakini akaongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu kwani uandikishaji utafanyika kama ulilovyopangwa.
“Unajua sikuwa na taarifa hizo kwa sababu nilikuwa katika kikao na wenyeviti wenzangu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kama kweli limesitishwa, itakuwa ni mchakato mdogo wa maandalizi haujakamilika. Ila niwatoe hofu wakazi wa mkoa huo uandikishaji utafanyika kama ulivyopangwa,” Jaji Lubuva.