Kamati ya kudumu ya bunge ya katiba, sheria na utawala bora imeitaka takukuru kuongeza nguvu katika kufanya uchunguzi maalum wa tuhuma za rushwa katika vocha za pembejeo za kilimo, maliasili pamoja na kukamilisha uchunguzi kuhusu sakata la akaunti ya tegeta escrow ili watakaobainika wafikishwe mahakamani mapema kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mh Samson Rweikiza akisoma taarifa ya kamati bungeni mjini Dodoma imeitaka serikali kuiwezesha kikamilifu takukuru kwa kuipatia nyenzo na rasilimali watu wenye weledi na kuitengea bajeti ya kutosha huku ikiitaka serikali kuhakikisha chuo cha uongozi kinaingiza mtaala wa maadili ya uongozi ili kupata viongozi wenye maadili.
Kwa upande wa hotuba ya msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni iliyosomwa na Mh Esther Matiko kuhusu mapitio ya utekekelezaji wa bajeti ya matumizi ya ofisi ya rais mahusiano na uratibu imeitaka serikali kushughulikia mifumo holela ya kodi ambayo imesababisha wafanyabiashara kuendelea kugomea mashine za EFD na kusababisha migomo ya mara kwa mara.
Wakichangia makadirio ya matumizi ya fedha za ofisi ya rais, tume ya mipango pamoja na wizara ya ofisi ya rais, menejimenti ya utumishi wa umma baadhi ya wabunge wameitaka serikali kuipa takukuru meno tofauti na sasa ambapo wanatumia mlolongo mrefu badala ya kuzipeleka mahakamani moja kwa moja huku wengine wakielezea tatizo la ukosefu wa fedha kwenye taasisi zilizopo chini ya ofisi ya rais hali iliyosababisha kutokuelewana kwa kile kilichodaiwa uombaji wa taarifa kwa upendeleo.
Hata hivyo kadri siku zinavyosogea idadi ya wabunge ndani ya ukumbi wa bunge inazidi kupungua pengine kwa kile kinachodaiwa kuwa ni homa ya uchaguzi mkuu ambapo baadhi ya wabunge wako kwenye majimbo yao.