Vijana wa chadema wafanya matembezi kuelekea Butiama ili kuhamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura

Baadhi ya vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kutoka wilaya za Nyamagana, Magu, Busega na Bunda wameanza matembezi ya siku sita kuelekea katika kijiji cha Butiama kwenye kaburi la hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kuwahamasisha watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Matembezi haya ya vijana wa Chadema yameanzia eneo la igoma jijini Mwanza, mahali ambako mwaka 1967, Mwalimu Julius Kambarage nyerere aliishia baada ya kutembea kwa miguu kutoka mwitongo, Butiama mkoani Mara akiunga mkono azimio la Arusha.
 
Kiongozi wa msafara huo George Charles ambaye ni mwenyekiti wa baraza la vijana wa Chadema (Bavicha) kata ya igoma anasema lengo la matembezi hayo ya zaidi ya kilometa 260 pamoja na mambo mengine ni kupinga ufisadi, mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino, vikundi vya kihalifu vilivyoibuka jijini Dar es Salaam maarufu kama panya road, ambapo wamelitaka jeshi la polisi kutowazuia na safari yao kwa vile matembezi hayo ni ya amani kwa ajili ya kumuenzi baba wa taifa.
 
Baadhi ya vijana wanaoshiriki matembezi hayo wanasema wameamua kufanya hivyo kwa dhamira njema ili kuwahamasisha watanzania kujitokeza kujiandikisha na pia kupinga uporaji wa raslimali za taifa unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watu wachache waliokabidhiwa dhamana ya uongozi na kusababisha ufa mkubwa kati ya wenye nacho na wasionacho huku wananchi walio wengi wakiendelea kukabiliwa na umaskini.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo