Kufuatia kukithiri kwa migogoro ya ardhi mkoani Mwanza, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemsimamisha
kazi Ofisa Ardhi Manispaa ya Ilemela, Asubuhi Otieno.
Otieno anatuhumiwa kujipachika cheo cha kamishna
ardhi mteule na kubadili hati miliki ya ardhi namba 147 Kitalu C, mali
ya marehemu Almas Chande na kummilikisha Kabinga Mkama.
Pia, Ofisa Mipango Miji Nyamagana, Kazi Maduhu na
Ofisa Ardhi wake, Sylvester Salvatory hatima yao inasubiri ushauri wa
kamati iliyoundwa na Waziri Lukuvi kutokana na malalamiko mengi ya
wananchi kuelekezwa kwa watumishi hao.
Uamuzi wa kumsimamisha Otieno ulifikiwa kwenye kikao cha majumuisho ya ziara ya siku tatu ya waziri huyo jijini Mwanza juzi.
Lukuvi aliunda kamati maalumu itakayochambua kwa
mwezi mmoja barua za malalamiko 600 kutoka Manispaa ya Ilemela, 800 za
Nyamagana na kumpa ushauri.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kusimamishwa kwa
Otieno, mama mzazi wa marehemu Chande, Amina (78) aliwasilisha barua ya
Desemba 17, 2013 ikimtaarifu kubadilika kwa mmiliki wa ardhi kutoka kwa
Chande kwenda kwa Mkama.
Hali hiyo ilimshtua Lukuvi na kulazimika kumhoji ofisa huyo kama anaitambua barua hiyo.
Otieno alikiri kufanya hivyo na akatakiwa kuisoma mbele ya hadhara na yeye akaisoma kinyume na ilivyoandikwa.
Waziri Lukuvi hakuridhika ikabidi aisome mwenyewe
na kukuta kilichosomwa ni tofauti na kilichoandikwa. Otieno alipoulizwa
sababu za barua hiyo kutokuwa na muhuri wa kamishna, alikosa majibu na
kusababisha umati wa watu kumzomea huku wakisema: “Bora umefika mwenyewe
acha uyaone”.
Kuhusu Manispaa ya Nyamagana, Sylvester Salvatory
anadaiwa kuvamia kiwanja cha Ester Jerome chenye namba 137 Kitalu X eneo
la Kapripoint na kukiuza kwa mtu mwingine, huku akimwomba mmiliki
halali Sh1 milioni ili amsaidie kukirejesha mikononi mwake.
Pia, Salvatory anadaiwa kumwomba Ester Sh300,000
kwa ajili ya kumpelekea Ofisa Mipango Miji, Kazi Maduhu ili amsaidie
kumpatia hati miliki nyingine na kwamba, alimpa fedha hizo na kuahidiwa
kupelekewa stakabadhi ambazo hajakabidhiwa hadi sasa.
Maelezo hayo yalimfanya Waziri Lukuvi kumsimamisha
Salvatory na kumhoji tena kama anakifahamu kiwanja hicho, naye alikiri
kukifahamu lakini akashindwa kutoa sababu za kumtoza fedha bila kumpatia
stakabadhi mama huyo.
“Natetemeka kwa sababu ya ukweli, naona unaniuliza maswali ya
kunionea, kama ni kuwajibika nitawajibika kwani sikuzaliwa kuwa Ofisa
Ardhi Mwanza, ifahamike kuwa maisha ni popote,” alisema Salvatory huku
akibubujikwa machozi.
Waziri Lukuvi alisema Wilaya ya Kinondoni
inaongoza kwa migogoro ya ardhi, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza. Alisema
migogoro hiyo inasababishwa na maofisa ardhi ambao aliapa
kuwashughulikia.
Kikao hicho kilishirikisha zaidi ya wenyeviti 200
wa Jiji la Mwanza, kila mmoja aliwasilisha kabrasha lenye malalamiko
kwenye mitaa yake.