Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia wahamiaji haramu 64 kutoka nchini Ethiopia waliokamatwa katika kijiji cha mkoka wilayani chemba wakiwa safarini kuelekea nchini Malawi ambapo mmoja kati yao amefariki dunia kutokana na njaa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Sacp David Misime akithibitisha kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu amesema waliingia kutokea Tanzania kupitia mkoa wa Kilimanjaro wakiwa wamepakiwa kwenye gari
aina ya Mitsubish fuso lenye namba za usajili T 353 ambalo lilikuwa
limebeba magodoro 55 ili kuwaficha wahamiaji hao ambapo gari hilo
lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Othmani
Mteketa liliharibika njiani na ndipo wananchi wakabaini kuwepo kwao na
kutoa taarifa polisi.
Aidha kamanda Misime ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa
taarifa pindi wanapokuwa na mashaka na watu katika maeneo yao ili
kuwabaini mapema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya
ulinzi na usalama wilaya ya Dodoma mjini Betty Mkwasa ametoa wito kwa
watu wa mipakani kuwa makini na watu wanaoingia na kutoka nchini kwani
haiwezekani watu wakatoka Kilimanjaro hadi Dodoma bila kujulikana.