Umoja wa Makanisa mkoani Tanga umeishauri serikali kusogeza mbele zoezi la kupiga kura ya maoni kuhusu rasimu ya pili ya katiba Pendekezwa kufuatia muda wa mwezi mmoja uliotolewa kwa ajili ya wananchi kuisoma hautoshi sanjari na nakala zilizotolewa kwa ajili ya wananchi kujisomea kuwa chache.
Wakitoa tamko rasmi kwa serikali kuhusu zoezi la katiba hiyo,viongozi wa madhehebu ya makanisa yote mkoa wa Tanga wamesema ni vyema serikali ikasogeza mbele kabla ya siku ya mwisho ya mwezi April haijawadia ili kutoa nafasi ya kutosha ya kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.
Aidha katika kikao hicho kilichoshirikisha viongozi wa makanisa yote nchini mkoani Tanga baadhi yao walilalamikia mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi na kuiomba serikali ijenge umoja wa kitaifa kwa kuimarisha Demokrasia zikiwemo za kidini kama alivyofanya mwasisi hayati Mwalimu Jullius Nyerere.
Zoezi la kupiga kura ya maoni katika katiba pendekezwa nchini linatarajiwa kufikia ukomo aprili 30 mwaka huu ambapo wananchi walioingizwa katika Daftari kuu watapata fursa hiyo kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).