Basi la Magereza lililokuwa limebeba wafungwa/maabusu
limeshambuliwa kwa risasi na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi leo
(July 2) katika eneo la Mikocheni, Dar es Salaam.
Akizungumza, Kamanda wa polisi Mkoa wa Kipolisi wa
Kinondoni, Camellius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kueleza kuwa jeshi la polisi limeanza kufanya uchunguzi.
Kamanda Wambura amesema ni mapema kutaja nia ya watu hao wenye silaha
waliovamia gari hilo kwa kuwa wanaweza kuwa na nia tofauti kabisa na
fikra za haraka.
“Tunafanya uchunguzi ambao utatufikisha mahali tuweze kubaini ni
nini. Inawezekana pengine kuna wahalifu walikuwa katika harakati za
uhalifu ghafla wakaona basi lile ambalo lina askari wazuri wenye silaha
wakaanza kulishambulia…inawezekana. Au inawezekana vingine vyovyote
ambavyo hatuwezi kufikiri wala kubaini.” Kamanda Wambura
Ameeleza kuwa hakuna maabusu yoyote aliyeweza kutoroka katika tukio
hilo na kwamba madhara yaliyotokea kwenye gari hilo sio makubwa. Amesema
bado hajapata taarifa yoyote ya uharibifu wa mali au upotevu wa mali
uliotokea katika eneo hilo kufuatia tukio hilo.
Akizungumzia watu waliojeruhiwa katika tukio hilo, Kamanda Wambura
amewataja watatu waliopata majeraha kuwa ni dereva wa basi hilo,
mahabusu mmoja na askari mmoja wa kike.
“Kuna baadhi wana michubuko, wale wawili ambao ni dereva na
mahabusu mmoja. Lakini kuna askari wa kike ambaye yeye ana majeraha
kwenye kifua upande wa kulia. Lakini ni nini kimesababishia michubuko
ile hatuwezi kujua kama ni vioo ama ni purukushanai wamejichubua mle
ndani au vitu gani.” Amefafanua.
Kwa undani wa habari hii, usikose kusikiliza taarifa ya
habari ya 100.5 Times Fm leo Moja na dakika 45 usiku, na pia katika
kipindi cha The Jump Off kinachoanza saa mbili kamili hadi saa nne
kamili usiku.
CHANZO: TIMES FM