ABIRIA 57 wa basi la Osaka lililokuwa linatoka Bukoba kwenda Dar es
Salaam wamenusurika kifo baada ya basi hilo kugonga tela la lori
lililokuwa limeegeshwa kutokana na kuwa bovu na kutumbukia mtaroni.
Ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu Dodoma/Morogoro eneo la
Chuo cha Biashara (CBE) Kata ya Makole Manispaa ya Dodoma kwenye
makutano ya barabara maarufu kama kona ya Dodoma Inn, majira
yanayokaribia saa sita usiku.
Imeelezwa kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T. 197 BUS
Scania, Said Chaupendo Mshana (33) aligonga tela hilo lenye namba za
usajili T. 533 BNM la gari lenye namba za usajili T. 426 BMJ Scania
lililokuwa likiendeshwa na Idd Juma (41) lililokuwa limeharibika, kabla
hajatumbukia mtaroni na kujeruhi abiria mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kwamba basi
hilo la Osaka baada ya kushusha abiria stendi kuu ya mabasi Dodoma
liliondoka likiwa katika mwendokasi na kushindwa kusimama pamoja na
kusimamishwa na askari wa usalama barabarani waliokuwa kwenye eneo
ambalo lori limeharibika.
“Kutokana na mwendokasi, aliligonga tela kisha kutumbukia mtaroni
pembeni mwa barabara katika uzio wa Chuo cha Biashara (CBE) na
kusababisha majeruhi kwa abiria mmoja aliyefahamika kwa jina la Justa
Trazias mwenye miaka 19, mkazi wa Ubungo River side Dare es Salaam
ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa Dodoma kwa matibabu na hali
yake inaendelea vizuri,” alisema Kamanda Misime.
Kamanda Misime alisema uchunguzi wa awali unaonesha kwamba chanzo cha
ajali hiyo ni uzembe wa dereva, mwendokasi na kukataa kutii amri ya
askari aliposimamishwa kisha kushindwa kulimudu gari na kusababisha
ajali hiyo.
Kamanda huyo ametoa mwito kwa madereva kuwa na udereva wa kujihami na
wenye kuchukua tahadhari na kufuata sheria kwa kutokiuka agizo la
mabasi kutotembea baada ya saa sita usiku.
“Kwa muda huo alitakiwa walale stendi ya mabasi Dodoma na ndiyo maana
aliposimamishwa na askari alikataa kusimama na matokeo yake
akasababisha ajali hii,” alisema Kamanda Misime.