Katika
juhudi za kukomesha matukio ya kihalifu yaliyoibuka hivi karibuni ya
kuwaua na kuwajeruhi ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwa
visingizio vya imani potofu za ushirikina, Jeshi la Polisi nchini,
limeendelea kupambana na vitendo hivyo vya kikatili ili kuhakikisha
kwamba matukio kama hayo hayaendelei na wenzetu wenye ulemavu wa ngozi
hawaishi kwa hofu ya kutendewa uhalifu.
Ni
katika juhudi hizo, Jeshi la Polisi nchini linaendelea na Operesheni
kali katika mikoa yote kuhakikisha kwamba mtandao mzima unaojihusisha
kwa aina moja ama nyingine na matukio hayo unakamatwa wakiwemo waganga
wa jadi wapiga ramli chonganishi.
Aidha,
Jeshi la Polisi nchini hadi sasa katika oparesheni inayoendelea
limewakamata wapiga ramli chonganishi 225 katika mikoa ya Tabora, Geita,
Mwanza, Simiyu, Shinyanga Kagera, Katavi na Rukwa, ambapo kati yao 97
tayari wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukutwa na
vifaa vya uganga ambavyo vingine ni nyara za serikali kama vile ngozi ya
Kenge, meno ya Ngiri, mikia ya Tumbili, miguu ya ndege, mikia ya
nyumbu, ngozi ya simba, ngozi ya fisi, ngozi ya digidigi na wengine
kufanya uganga bila kibali.
Tatizo
kubwa linalosababisha uhalifu huu kuendelea kujitokeza ni imani mbaya
na potofu za kuamini ushirikina. Bado wananchi wetu wengi wanaamini
katika ushirikina unaosababisha uhalifu kama huu na ule wa mauaji ya
vikongwe kuendelea kutokea. Rai kwa wananchi ni kwamba waache tabia
hizo/imani potofu za kishirikina ili matukio haya yakomeshwe.
Tunawaomba
wananchi watupatie taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa
hao na wale wanaoeneza imani potofu za kishirikina.
Jeshi
la Polisi nchini linazidi kutoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo
viongozi wa dini, asasi za kiraia, wanasiasa, wazee wa kimila,
wanahabari na wananchi kwa ujumla, kuendelea kuielimisha jamii kuachana
na imani za kishirikina ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya Taifa
letu.
Imetolewa na;
Advera John Bulimba - SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
11 March, 2015.