Mwenyekiti
wa taifa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Mh. Freeman Mbowe
amesema njia pekee ya kukiondoa chama cha mapinduzi madarakani katika
uchaguzi mkuu ujao ni viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya
wananchi (Ukawa), kuweka kando maslahi binafsi ya vyama vyao na
kusimamisha mgombea mmoja katika kila nafasi ya uongozi, huku akionya
kuwa endapo atatokea kiongozi yeyote ndani ya Ukawa mwenye uchu wa
madaraka ni afadhali akatengwa kama msaliti.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa manispaa ya Tabora katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Town School, kata ya gongoni
mjini Tabora, mwenyekiti huyo mwenza wa Ukawa, amesema mambo
yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa baadhi ya
wagombea wa vyama vinavyounda Ukawa, ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR –
mageuzi na NLD kugombania baadhi ya maeneo kwa ajili ya tamaa na uchu wa
madaraka yanapaswa kuwa ni funzo kwa uchaguzi ujao wa mwezi oktoba
mwaka huu.
Mh. Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni
na mbunge wa hai, ameeleza kusikitishwa na hali ya umaskini
inayowakabili wakulima wa mazao mbalimbali nchini, wakiwemo wa zao
tumbaku mkoani Tabora na pamba katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga
na Simiyu kutokana na kulipwa bei ndogo jambo ambalo limesababisha hata
baadhi ya viwanda vya nguo nchini kufa kifo cha kawaida, huku serikali
ikishindwa kuvifufua na badala yake imeendelea kukaribisha wawekezaji wa
nje kuja nchini kuwekeza kwenye migodi ya madini na wananchi kuambulia
mashimo.
Kwa upande wake, naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum
Mwalimu amesema kwamba kwa muda mrefu watanzania wamekuwa wakidanganyika
kwa kudhani kuwa uongozi mbovu ni matokeo ya viongozi waliowachagua na
kusahau kuwa tatizo sio viongozi wanaotokana na chama cha mapinduzi,
bali ni chama chenyewe, dhamira yake na mifumo waliypoiweka katika
kutumikia watanzania.