Tarehe 08/03/2015, Dr. Wilbroad Slaa Katibu Mkuu wa Chadema kupitia kwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Ndugu Mabere Marando alitoa tuhuma kwa Serikali na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuwa wanapanga njama za kumdhuru Katibu Mkuu huyo wa Chadema.
Kimsingi
tuhuma hizi ni za kipuuzi, lakini uongo huu usipojibiwa unaweza
kugeuzwa kuwa ajenda na Chama hiki cha Chadema kwa kukosa ajenda zingine
za maana. Hakuna asiyejua kuwa Chadema kwa sasa kinapumulia mashine,
hivyo maneno na matendo yao kwa sasa lazima yalenge kujaribu kujinasua
na balaa la kufa kwa chama chao.
Ni
vizuri Watanzania wakakumbuka historia ya tuhuma lukuki zilizowahi
kutolewa na Katibu Mkuu huyu wa Chadema toka aanze siasa na ambazo zote
zilikuja thibitika kuwa ni za uongo. Hapa nitawakumbusha baadhi.
Akiwa
Singida katika kampeni za Urais za mwaka 2010, Dk. Slaa aliwatangazia
wananchi mkutanoni kwamba walikuwa wamekamata lori kubwa la mizigo
(semi-trela) lililojazwa karatasi za kura za Urais zilizokuwa tayari
amepigiwa kabisa mgombea Urais wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete.
Katika
kuonyesha kwamba alikuwa na uhakika wa jambo hilo, alisoma hadi namba
za lori hilo na tela lake kutoka kwenye karatasi aliyokuwa ameshika
mkononi, kisha akasema kuwa lori hilo lilikamatwa katika mji mdogo wa
Tunduma, mkoa wa Mbeya wakati likiingia nchini kutoka Lusaka, Zambia.
Lakini
baada ya polisi kuchukua hatua za haraka wakitumia namba za lori na
tela lake alizokuwa amezisoma na kulikamata, kisha wakalipekua hadharani
huku wananchi wakishuhudia palepale Tunduma, kilichokutwa ndani ya lori
ilikuwa shehena ya vipodozi vya kina mama na sabuni za manukato.
Baada
ya siku chache huku akiwa amesahau yote, Dk. Slaa akatangaza tena kuwa
mgombea Urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alikesha katika hoteli ya
Lakairo, Mwanza akiweka mikakati ya kuiba kura siku ya uchaguzi huo wa
mwaka 2010 ili ashinde. Siku chache alisema kura zimeingizwa na
zimeshapigwa, hapa amesahau anadai ndio kwanza mpango unapangwa.
Aliwataja
watu wengine aliodai walikuwa pamoja na Rais Kikwete kuwa ni aliyekuwa
Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Mkurugenzi wa Hoteli hiyo iliyopo
katika jiji la Mwanza, Lameck Airo.
Lakini
wakati Dk. Slaa akisema uongo huo, Rais Kikwete siku nzima na usiku
wake wote alikuwa Mtwara akiendelea na kampeni zake za Urais.
Hata
Rostam Aziz naye kwa siku hiyo pamoja na usiku wake wote alikuwa Igunga
akiendelea na kampeni zake za Ubunge, na pia hata Airo naye siku nzima
na usiku wote huo alikuwa jimboni kwake Rorya akifanya kampeni zake za
kugombea Ubunge.
Baada
ya kushindwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk. Slaa aliwaambia waandishi
wa habari kwamba alikuwa na ushahidi wa matokeo ya Urais ya kituo kwa
kituo ya nchi nzima yakionyesha kuwa alishinda.
Akasema,
chama chake kingeyasoma hadharani na kuwakabidhi waandishi wa habari
ili wananchi waujue ukweli kuwa alidhulumiwa ushindi wake, kazi
iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na haki yake akapewa aliyekuwa
mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Lakini
kwa vile alikuwa akiwatangazia uongo wananchi, Dk. Slaa hadi leo
hajawahi kuyasoma matokeo hayo ya kughushi, badala yake alipowaita tena
waandishi wa habari akatangaza kuwa Tanzania isingetawalika mpaka
arudishiwe haki yake. Hapo ndipo ghasia zikiwemo za mauaji za Chadema
zilipoanza hadi leo.
Januari,
2011 aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa na mkanda
unaothibitisha kuwa mauaji ya Januari 5, mwaka huo yaliyofanyika katika
jiji la Arusha kutokana na maandamano ya vurugu ya wafuasi wa Chadema
yalifanywa kwa makusudi na polisi, na kwamba wafuasi wake hawakufanya
fujo wala vurugu zozote.
Alisema
mkanda huo angeuonyesha mbele ya waandishi wa habari ndani ya siku tatu
au mbili baada ya Polisi Makao Makuu, kuonyesha unaothibitisha kwamba
wafuasi wa Chadema walifanya vurugu ikiwemo kutaka kuvamia Jengo la
Makao Makuu ya Polisi la Mkoa na kupora silaha zilizokuwa humo,
wawafungulie wahalifu waliokuwa ndani na kulichoma moto jengo lenyewe.
Lakini
tokea kipindi hicho hadi sasa ikiwa tayari imeshapita miaka minne, Dk.
Slaa siyo tu ameshindwa kuuonyesha mkanda huo “ndani ya siku tatu ama
mbili” alizokuwa ameahidi, bali amethibitisha kwamba alichosema kwa
Watanzania ulikuwa ni uongo na uzushi.
Mwaka
2011, Dr. Slaa alikwenda mbali kwa kuzusha kwenye mkutano wa hadhara
kuwa aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati huu Brig. Gen. mstaafu
Yohana Balele amefariki dunia.
Akajaribu
kuwaaminisha wananchi pale kuwa ni kweli, baadae ikagundulika kuwa Mkuu
huyo wa Mkoa ni mzima na wala haumwi. Haikujulikana mara moja sababu za
Dr. Slaa kumzushia kifo Mkuu huyo wa Mkoa.
Julai
2012, Dr. Slaa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika walizusha kwamba
wanafuatiliwa na baadhi ya Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ili
wauawe, lakini walipotakiwa kupeleka ushahidi wao katika vyombo vya dola
ili kusudi watuhumiwa wachunguzwe na hatimaye wakamatwe na kuruhusu
Sheria ichukue mkondo wake, wote waligoma na kudai hawapo tayari
kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Waliendelea
na msimamo huo hata pale Dk. Slaa alipolazimishwa kwenda Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi na kuhojiwa, lakini akashindwa kutoa uthibitisho wake
mwenyewe wala wa Mnyika kwa sababu walidai suala hilo limezungumzwa
katika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema.
Mwaka
2012, Dr. Slaa akiwa ziarani Ifakara wilayani Kilombero mkoa wa
Morogoro, alidai kuwa CCM imeingiza silaha kutoka nje ya nchi kontena
zima, ili zitumike kuwadhuru viongozi wa Chadema, jambo ambalo hata
hivyo hadi leo ameshindwa kulitolea uthibitisho wala kielelezo chochote.
Wanaomfahamu
vizuri endapo ingekuwa kweli angeita waandishi wa habari, akatoa
ushahidi wake na kuwakabidhi ili wautumie kuandika madai hayo, lakini
kwa sababu ulikuwa ni uongo ndiyo maana hakutoa karatasi yoyote hadi
leo.
Juzi
bila aibu anaibuka na tuhuma zingine za eti kutaka kuuawa. Kupanga
kumdhuru Dr. Slaa, ili CCM ipate nini kwa kudhurika kwake? Kwa umri
wake, afya yake na kadhalika, kwa nini CCM ipange kumdhuru mzee huyu?
Huu ni mwendelezo wa tabia yake ya kuzusha mambo ya uongo kila anapoona
anachuja kisiasa. Ni busara kwa umri wake akatumia muda wake mwingi
KUMRUDIA MWENYEZI MUNGU.
Lakini hata mtu aliyetumika kuufikisha uongo huo kwa umma, naye ana historia ya kuzusha mambo na kusema hata asiyoyaamini.
Marando
aliwahi kuitisha kikao na waandishi wa habari na kudai Katibu wa
Itikadi na Uenezi alifaidika na pesa za EPA, alipobanwa na mteja wake
aliyekuwa akimtetea mahakamani kwa kesi hiyo hiyo ya EPA, akaruka yale
matamshi yake kwa maandishi na kudai ilikuwa ni shinikizo la Chama chake
kusoma yale maneno lakini hata yeye hayaamini.
Lakini
ni Marando huyu huyu ambaye akipanda kwenye majukwaa ya siasa anadai
swala la EPA ni ufisadi mkubwa sana kwa nchi na akishuka tu jukwaani,
anakimbia mahakamani kwenda kuwatetea watuhumiwa hao hao wa EPA
aliowaita majukwaani mafisadi wa EPA. Mzee huyu naye ni mnafiki.
Hebu
tujiulize, ni lini Mabere Marando aliacha rasmi kazi yake ya awali ya
ukachero mpaka aaminike leo kufanya kazi afanyayo? Nani alimtumia
kujaribu kusambaratisha chama cha NCCR-Mageuzi miaka ya mwanzo ya mfumo
wa vyama vingi nchini? Hivi ni kweli Marando ni wa kuaminiwa leo?
Natoa
wito kwa Watanzania bila kuingilia utaratibu wa Sheria na vyombo vya
Serikali kufuatilia uongo huu mpya, Watanzania nawaomba wampuuze na
kupuuza uongo huu. Usitupotezee muda, tuendelee na mambo ya msingi ya
kujenga nchi yetu.
Nimshauri
pia babu yangu Dr. Slaa, kwa umri wake, wenzake wakifikisha umri huu wa
uzee wanatumia muda wao kumrejea Mwenyezi Mungu badala ya yeye
kuendelea kutunga uongo na uzushi kila kukicha. Namwomba mwenyezi Mungu
ampe kuiona busara hiyo.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU -CCM YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI