Mahakama Kuu ya Tanzania, jana imetupilia mbali
shauri lililofunguliwa na Zitto Zubeir Kabwe mwaka jana, akipinga kikao
cha Kamati Kuu ya Chadema kumjadili, akikitaka chombo hicho cha sheria,
kukielekeza chama chake, kusubiri kwanza rufaa yake aliyokuwa amekata
katika Baraza Kuu.
Mahakama iliyoketi chini ya Jaji Mziray, ilikubaliana na hoja za
mawakili wa Chadema, waliosema kuwa ufunguaji wa kesi hiyo ulikiuka
baadhi ya vifungu vya sheria na hivyo kumtaka mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Baada
ya hukumu hiyo, Zitto Kabwe amesema hakuwa na wito wa mahakamani jana na Jaji aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo amehamishiwa Tabora,
hivyo mwanasheria wake ameenda kufuatilia mazingira ya hukumu
hio.
Wakati Zitto akifungua kesi hiyo Januari mwaka jana, tayari Chadema ilikuwa imewafukuza uanachama Dr. Kitilya Mkumbo na Samson Mwigamba ambao pamoja na Zitto, walituhumiwa kupanga njama za kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya chama hicho.
Zitto alikuwa akitetewa na wakili Albert Msando wakati Chadema iliwakilishwa na Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Mallya.