Mahakama
ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, juzi imemhukumu mwanamume mmoja Festo
Domisian (30), mkazi wa wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, kutumikia
kifungo cha miaka 60 jela pamoja na kuchapwa viboko 12, baada ya
kupatikana na hatia ya kubaka wasichana wawili kwa zamu akiwa na kisu na
kumjeruhi mmoja wao.
Hukumu
hiyo ilitolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Hamad Said Kasonso, baada ya
kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa
mashitaka.
Awali
ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa Polisi Inspekta
Hamza Mdogwa, kuwa mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo Agosti 14 mwaka
jana, majira ya saa 7:00 usiku katika kijiji cha Busambara, kata ya
Kibara, wilayani Bunda.
Mdogwa
alisema kuwa mshitakiwa huyo aliwaingilia ndani ya nyumba walimokuwa
wamelala wasichana hao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu ya umri wao
kuwa mdogo na kuwatishia kwa silaha aina ya kisu na kuanza kuwabaka kwa
zamu.
Alisema
kuwa kabla ya kuanza kuwabaka wasichana hao, alivunja mlango wa nyumba
yao na kwamba alimjeruhi mmoja wao kwa kumchoma na kisu sehemu ya begani
na shingoni na kisha akaanza kumbaka na baada ya kumaliza haja yake
akambaka msichana wa pili na kisha akatokomea kusikojulikana.
Aliongeza
kuwa kwa vile walalamikaji hao walimtambua kwa sura mshitakiwa huyo
walitoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho na wananchi
wakafanikiwa kumkamata na kumpeleka Polisi.
Akitoa
hukumu hiyo Hakimu Kasonso alisema kuwa kosa la kubaka msichana wa
kwanza ni kifungo cha miaka 30 jela na kosa la kubaka msichana wa pili
pia ni kifungo cha miaka 30, na kwamba adhabu zote zinakwenda kwa
pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko
12, siku ya kuingia sita na siku ya kumaliza adhabu yake anachapwa
vingine sita.
