Jeshi
la polisi mkoani Mwanza, linawashikilia watu 14 kwa tuhuma za kuhusika
na tukio la utekaji nyara wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Pendo Emanuel
wa kijiji cha ndami wilayani kwimba lililotokea Desemba 27 mwaka jana.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa mulongo akizungumza wakati wa hafla
ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya za Misungwi, Kwimba na Sengerema
amesema kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wamo waliohusika kwenye utekaji
wa mtoto huyo pamoja na wale waliomuhifadhi kwenye hoteli moja jijini
Mwanza kabla ya kumsafirisha kwenda kusikojulikana.
Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la kuwaapisha wakuu hao wapya wa
wilaya hizo tatu za mkoa wa Mwanza, ambao ni Pily Moshi wa Kwimba,
Zainabu Telack wa Sengerema pamoja na Mwajuma Nyiluka wa Misungwi, mkuu
huyo wa mkoa wa Mwanza ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama ya mkoa huo akabainisha zilizofikiwa katika kuwasaka watu
wanaotuhumiwa kumteka nyara mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Pendo Emanuel
na kutokomea kusikojulikana.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa Mwanza
Alfred Kapole pamoja na katibu wa chama hicho mkoani humo Enos Tuju
wameendelea kupaza sauti zao kwa kuiomba serikali kudhibiti vitendo vya
mauaji ya albino yanayotokea Mwanza.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza Acp Japhet Lusingunaye
akawa na neno juu ya hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi kuhusiana
na mauaji ya watu takribani 16 wenye ulemavu wa ngozi yaliyotokea katika
mkoa wa Mwanza peke yake.