MAAJABU yanadaiwa kujitokeza kwenye maziko ya aliyekuwa staa wa Bongo Fleva kutoka Kundi la Chamber Squad, Moses Bushagama ‘Mez B’, ambapo jeneza lililobeba mwili wake lilidaiwa kugoma kuingia kaburini huku Wana-chamber wenzake, Haji Malick ‘Noorah’ na Athumani Kabongo ‘Dark Master’ wakiwa hoi baada ya kuishiwa nguvu na kusababisha watu wataharuki na wengine kuingiza imani za kishirikina.
Kuhusu kaburi, ilidaiwa kwamba moja ya changamoto katika kuupumzisha mwili huo ni jeneza kugoma kuingia kaburini na kuwafanya wachimbaji kuongeza ukubwa (upana) wa shimo ambao ulisababisha usumbufu.
Shuhuda wa Amani alidai kwamba, siku ya maziko hayo kulitokea hali ya sintofahamu, hasa baada ya kufikisha mwili wa marehemu eneo la makaburi, hasa changamoto na taharuki ilikuja baada ya jeneza kubana walipotaka kuzika hivyo wakalazimika kuliweka pembeni na kuanza kuchimba upya.
“Ukiachilia mbali hilo, pia kulikuwa na ishu ya kuishiwa nguvu kwa Noorah na Dark Master ambao muda mwingi walikuwa wakijisikia kizunguzungu,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumzia ishu hiyo, Dark Master alisema kwamba, wanamshukuru Mungu harakati za maziko zilifanikiwa, isipokuwa kulikuwa na changamoto za hapo na pale likiwemo suala la jeneza kushindwa kuingia kaburini hali iliyowalazimu kusimamisha shughuli hiyo kwa muda na kupanua zaidi kaburi.
Alisema ishu nyingine ilimpata yeye na Noorah ambapo muda mwingi walikuwa wakipatwa na kizunguzungu na kuishiwa nguvu, kiasi cha kupoteza fahamu jambo ambalo si la kawaida kwa upande wake.
“Suala la kuishiwa nguvu halikuishia kwangu tu bali hata Noorah naye lilimkumba sana, ingawa yeye alipata msaada wa kuwa karibu na watu kwa muda wote tofauti na mimi ambaye nilikuwa nikizidiwa sana nakaa pembeni na naamka mwenyewe, namshukuru sana Mungu tumeweza kumsitiri mwenzetu pamoja na changamoto zote ambazo zimejitokeza,” alisema Dark Master.
Mez B ambaye alizaliwa mwaka 1982 alifariki dunia Februari 20, mwaka huu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua kikuu kwa muda mrefu.